NI Jumatatu nyingine tena napenda kukukaribisha katika safu hii maalum ya Ujasiriamali.
Wiki iliyopita tulizungumzia
namna ya kuanzisha biashara ya genge hivyo kuwaamsha walioamini kuwa
hawawezi, leo nitazungumza nanyi wasomaji wangu kuhusu biashara ya
kuzunguka minadani.
MNADA NI NINI?
Hii ni sehemu maalum iliyotengwa na
sekta husika, wananchi au wanakijiji wa sehemu husika kwa ajili ya
wafanyabiashara wa bidhaa tofauti na wanaotoka sehemu mbalimbali kwa
ajili ya kufanya biashara zao.
KWA NINI MNADANI?
Kwa kuwa mnadani kunakutanisha
wafanyabiashara wa sehemu na bidhaa mbalimbali, hata bei za bidhaa hizo
hutofautiana na hivyo hufanya kukutanisha idadi kubwa ya watu kama
wateja na wafanyabishara.
Biashara ya mnadani ni biashara nzuri
kwa mtu anayetaka kukuza mtaji wa biashara yake, kwa kuanza na mtaji
mdogo kwa kuzungusha kwenye minada mbalimbali mwisho wa siku unaweza
kuongeza mtaji na kuwa mkubwa kama utakuwa tayari katika kuzunguka
minada hiyo.
Biashara ya mnadani inakuwa na uhakika
kutokana na bidhaa uliyopeleka kwa walaji wako, kama utakuwa na uwezo wa
kupeleka dagaa kwa wahitaji wa dagaa ni dhahiri utaweza kufanya
biashara hiyo vizuri zaidi kwa sababu wateja wako ni wahitaji wa bidhaa
yako.
UZURI WA BIASHARA YA MNADANI
Inakupa fursa ya kuzunguka maeneo mengi
ya wilaya au mkoa husika au nchi husika, kufahamiana na watu mbalimbali
sambamba na kubadilishana uzoefu na ujuzi wa biashara yenu.
UPATIKANAJI WA FURSA MPYA
Kwa kuzunguka sehemu mbalimbali
minadani, kama wewe ni mjasiriamali mwenye malengo ya kufanikiwa katika
maisha yako, unaweza kupata fursa nyingi sana uwapo njiani ukielekea
maeneo ya minadani, hata kama siyo muda huo lakini ipo siku unaweza
kuwekeza au kufanya biashara kwa kutumia rasilimali ya aridhi au eneo
ulilodhamiria.
AINA ZA BIASHARA KATIKA MINADA
Zipo aina nyingi za biashara ambazo unaweza kuzifanya kwa kuzunguka kwenye minada.
Mojawapo ni biashara ya nguo za mitumba.
Tukutane wiki ijayo tuangalie sehemu ya pili ya mada hii kwa ajili ya wajasiriamali.

Note: Only a member of this blog may post a comment.