Na Sifael Paul
Habari mbaya iliyolifikia gazeti hili imeeleza kwamba, staa wa sinema
za Kibongo, Jacob Stephen ‘JB’ amenusurika kifo baada ya kudaiwa
kulishwa sumu na kujikuta katika hali mbaya kiafya kabla ya kukimbizwa
hospitalini.
Inadaiwa JB alizidiwa Jumamosi iliyopita alipoanza kulalamika kukatwa na tumbo, lakini wenzake wakachukulia poa na kumshauri kwenda kuchukua vipimo hospitali.
“Baada ya vipimo alipewa dozi akarudi nyumbani lakini asubuhi yake (Jumapili), hali ilizidi kuwa mbaya zaidi ndipo akakimbizwa Hospitali ya Marie Stopes (Mwenge, Dar).
Gazeti hili lilifika Marie Stopes na kuzungumza na baadhi ya wauguzi ambao walikiri JB kufikishwa hospitalini hapo akiwa katika hali mbaya.
“Madaktari waligundua kwamba alikuwa amelishwa sumu lakini mwenyewe alikuwa haelewi alichopewa kwa sababu alisema alikuwa amekula vitu mbalimbali tena sehemu tofauti,” alisema mmoja wa wauguzi hao ambaye aliomba hifadhi ya jina.
Akizungumza na gazeti hili kwa tabu, JB ambaye kwa muda mrefu alikuwa akizunguka mikoani kwenye kampeni za uchaguzi alisema kuwa alishangaa kujikuta akishindwa kuendelea na ratiba zake za kazi kufuatia kusumbuliwa na tumbo lililokuwa likimkata kabla ya kugundulika kuwa alilishwa chakula chenye sumu.
“Namshukuru Mungu naendelea vizuri lakini hali ilikuwa mbaya mno, bado sijaweza kutoka ndani naendelea na dozi,” alisema JB akiomba aendelee kupumzika.

Note: Only a member of this blog may post a comment.