Monday, September 7, 2015

Anonymous

GOOD NEWS: Sunday OLISEH Awapeleka…SAMATTA, KAPOMBE Ulaya!

Sweetbert Lukonge na Wilbert Molandi, Dar es Salaam
STRAIKA Mbwana Samatta na beki Shomari Kapombe, wanafaa kabisa kucheza kwenye Ligi Kuu ya England iliyojaa ubishi na ugumu wa aina yake, hiyo ni kwa mujibu wa Kocha wa Nigeria, Sunday Oliseh.
Mbali na wakali hao, Oliseh pia amesema kinda wa Azam FC, Farid Musa, naye ana uwezo wa ‘kutusua’ kwenye ligi hiyo. Maneno hayo yalimtoka gwiji huyo baada ya kushuhudia kikosi chake kikipelekwa puta na mastaa wa Stars na kulazimishwa sare ya bila kufungana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, juzi.
SAMATTA

Mbwana Samata.
Wakati Oliseh akiyasema hayo, Samatta tayari ameshapata dili la kucheza soka Ufaransa na amethibitisha kuwa mwakani atatimkia nchini humo na tayari ameshaanza kuwaaga wachezaji wenzake wa Mazembe anakolipwa mshahara wa dola 10,000 ambazo ni zaidi ya Sh milioni 20, kwa mwezi.

“Sikuamini kabisa kama Tanzania ingekuwa na wachezaji wazuri kama hao kwani waliwasumbua sana wachezaji wangu na ninashangaa kwa nini hawachezi soka Ulaya.
 
“Hata hivyo, mimi ni mtu wa soka na ninapenda maendeleo ya wachezaji wetu wa Afrika, ushauri wangu kwao ni kwamba wajitahidi kutumia mashindano haya kucheza kwa nguvu zao zote ili waweze kujitangaza na kuonekana machoni mwa mawakala wakubwa duniani.
 
“Pia shirikisho (TFF) linatakiwa kuwa na marafiki wengi nje ya Afrika ambao watakuwa msaada mkubwa kwa wachezaji wa Tanzania kupata nafasi za kucheza soka la Ulaya na Asia. Viongozi wajue kwamba mafanikio hutafutwa, hayakufuati ukiwa umekaa tu nyumbani kwako,” alisema Oliseh huku akiungwa mkono na Ofisa Habari wa Chama cha Soka Nigeria (NFA), Ademola Olajire.
Lakini Samatta, kabla timu yake ya taifa haijaivaa Nigeria, alitangaza rasmi kwamba amepata dili Ufaransa.

Awali, straika huyo aligomea kusajiliwa na Zamalek ya Misri iliyokuwa ikimhitaji kwa dau la Sh bilioni mbili, akasisitiza kuwa hataki kuendelea kuzunguka Afrika, badala yake anataka ‘kukata mawimbi’ Ulaya.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Samatta alisema kuwa mipango yote imekamilika na anachosubiria ni mkataba wake kumalizika ndiyo aondoke. Unatarajiwa kumalizika mwakani.
Samatta alisema kwa sasa hawezi kuitaja klabu hiyo ya Ufaransa atakayoitumikia mwakani lakini akakiri pia kuwa kuna timu nyingine kutoka Ubelgiji inayowania saini yake.

Aliongeza kuwa, kikubwa anashukuru ushirikiano mkubwa aliokuwa anaupata kutoka kwa bosi wake, Mose Katumbi na wachezaji wake wote kwa kipindi chote alichokuwa anaichezea Mazembe.
“Kiukweli kabisa nilipanga kuondoka muda Mazembe, lakini ikashindikana maana bosi wangu Katumbi alinihitaji kuendelea kumfanyia kazi kwenye klabu yake.

“Hivyo alinitaka niondoke mara baada ya mkataba wangu kumalizika.
“Nitaondoka Mazembe baada ya kupata klabu ya kwenda kuichezea Ufaransa ambayo nimefikia nayo muafaka, pia nimepata ofa nyingine kutoka Belgium (Ubelgiji) ambayo bado sijaifanyia maamuzi,” alisema Samatta.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.