Thursday, August 27, 2015

Anonymous

PART 2: Maajabu Ndani ya Basi la Dar-Arusha

IMG_7101ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
“Sawa. Mimi naitwa Rehema. Rehema Nyoni.”
Nilishtuka, maana mke wangu anaitwa Rehema Nyoni. Sasa yeye Rehema Nyoni yupi?
“Rehema Nyoni umeolewa?” nilijikuta nikimuuliza hivyo.
“Ndiyo. Mume wangu anaitwa Mussa, nina watoto wawili.”

Kama Ulimiss sehemu hiyoya iliyopita==>BONYEZA HAPA! SASA ENDELEA MWENYEWE…
Nilishtuka zaidi kwani mimi pia naitwa Musa.
“Mbona kama unashtuka anko kuna nini?” aliniuliza akiwa ananiangalia kwa macho ya kunishangaa kisha akaachia tabasamu.
“Wewe Rehema Nyoni wa wapi?”
“Kwani wewe unamfahamu wa wapi anko?”
“Mke wangu anaitwa Rehema Nyoni.”

“Si majina tu. Mbona si ajabu.”
Nilimwangalia yule binti mpaka tunapita Mlandizi. Yeye wakati huo macho yake yalikuwa mbele tu. Tulipokaribia Ruvu Darajani, niligeuza macho kuangalia nje ili niuone Mto Ruvu. Nikiwa naangalia nje, nikasikia sauti ya mwanaume mtu mzima pembeni yangu, alipokaa yule dada ikisema:
“Tunapita Mto Ruvu sasa.”

Niligeuka haraka sana kumwangalia nikijua ni yule mzee. Lakini nikakuta ni yule dada Rehema. Aliniangalia akaachia tabasamu na kuniuliza:
“Vipi? Mbona umeshtuka sana?”
“Nimesikia sauti kama ya mwanaume mzee.”
“Ikitokea wapi?” aliniuliza.

“Si kwako.”
“Ah anko. Mimi niwe na sauti ya kiume tena jamani!”
Niliacha kuangalia nje. Nikakaza macho mbele lakini jambo la ajabu jingine nililigundua. Abiria wote walikuwa wanafahamiana. Yule dada alianza kuongea na abiria tuliokaa nao mstari mmoja na waliulizana habari fulani za mtaani kwako.

Abiria wa nyuma yangu nao wakaanza kuongea, tena wakicheka na kumzungumzia mtu wanayemfahamu. Kifupi nilibaini kwamba, abiria walikuwa wakifahamiana.
Nilijiuliza mengi kuhusu hali ile. Nilijiuliza mbona basi nilipandia Ubungo, sasa kujuana kulitokea wapi? Na mbona hawakuonekana kujuana wakiwa wanapanda?
Kufika Chalinze, basi lilisimama kwenye mizani ya kuelekea Segera (kwa sasa imehamishwa). Baadhi ya abira walishuka, mimi sikushuka lakini Rehema yeye alishuka.

Tena baada ya kushuka nikamwona upande wa pili wa barabara akinunua mahindi ya kuchoma kisha akaenda kuingia kwenye kibanda kinachouza mananasi.
Mara, basi lilianza kuondoka huku yule dada akiwa bado ng’ambo ya barabara. Nilimhofia kuachwa nikamuita kwa sauti ya juu.

“Rehema unaachwa.”
Ghafla nikaguswa kwa nyuma.
“Anko Rehema gani tena, mbona mimi nimeshapanda muda mrefu?”
Niliangalia kule nje kwenye kibanda sikumwona. Halafu abiria wengine wakaanza kunicheka kwamba siko sawasawa.

“Jamani mimi niko sawa. Labda tu huyu dada ana mambo yake,” nilijitetea.
Safari iliendelea. Lakini nilianza kuhisi usalama wangu na maisha yangu yako hatarini. Ilifika mahali nikatoa tiketi ya lile basi kutoka kwenye kimkoba changu nilichokuwa nacho kwenye siti. Lengo lilikuwa kujiridhisha kama ni basi linalojulikana? Maana mimi nilikata tiketi tu pale Ubungo. Basi liliandikwa jina kwenye tiketi. Na ni basi linalojulikana sana.

Nilimwachia Mungu maisha yangu. Wakati basi linakaribia Mto Wami, nilimwamba Mungu tupite salama. Lakini nikiwa kwenye kumwomba Mungu kwa siri, nikaona basi linasimama pembeni mwa barabara. Dereva akasema:
“Jamani tunakula hapa. Dakika kumi tu. Baada ya hapa tunaendelea na safari. Sawa?”
Abiria wote walijibu sawa. Mimi peke yangu nilishtuka. Pale hapana hoteli wala nyumba, sasa anaposema tunakula, tunakula wapi.

Nilisimama, nikaangalia nje ili kuona kama naweza kuona jengo lolote. Hakukuwa na jengo. Lakini watu walishuka na kuzunguka gari. Kila aliyeshuka alizunguka gari. Na mimi nikashuka lakini kwa machale sana.
Kufika chini nikaona abiria wenzangu wapo vichakani wanajisaidia. Nikaenda na mimi. Nilimuuliza abiria mmoja mbona dereva kasema tule wakati hakuna hoteli? Akasema dereva alikosea, alimaanisha kujisaidia.
Hata hivyo, sikuridhika na majibu yake kwa kuwa, ile si sehemu sahihi ya kujisaidia. Sikuwahi kuona watu wanajisaidia eneo hilo.
Ili kuthibitisha hilo, hata mabasi mengine yalipokuwa yanapita, abiria walitushangaa sana.
Nilimtafuta Rehema, yule msichana lakini sikumwona. Na kwenye basi hakukuwa na abiria. Mimi ndiye nilishuka wa mwisho.

Mara, basi lilipiga honi. Lakini nilishangaa kuona abiria wenzangu wote wapo ndani ya basi. Kichakani nilibaki peke yangu.
Nilikimbia huku sauti ikiniambia nisiingie, nisubiri usafiri mwingine. Lakini nikasema ni uoga tu. Nikaenda kuingia. Siti zote zilikaa abiria. Rehema sikumkuta kwenye siti yangu.
“Jamani, huyu dada hajaingia,” nilisema kabla sijajiingiza kwenye siti kukaa upande wa dirishani.
Je, nini kiliendelea? Usikose kusoma wiki ijayo mkasa huu wa kweli unaoitwa Maajabu Ndani ya Basi la Dar-Arusha.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.