Saturday, June 13, 2015

Anonymous

MSUVA sawa, ila MAKATA, KADO mmh…!


Simon Msuva.
Nicodemus Jonas na Ibrahim Musa
TUZO ya Kocha Bora wa msimu uliopita ambaye ni Mbwana Makata na Kipa Bora Shaaban Kado, imeonekana kutokubalika na wadau wa soka nchini, lakini wakasema: “Kwa Msuva poa tu.”

Wadau hao wamebariki winga wa Yanga na Taifa Stars, Simon Msuva kutwaa Tuzo ya Mchezaji Bora akiwapiku Mrisho Ngassa na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’. Msuva pia ametwaa Tuzo ya Mfungaji Bora akifunga mabao 17.

Makata aliyekuwa akiifundisha Prisons ya Mbeya, juzi Alhamisi usiku aliwabwaga Hans van Der Pluijm wa Yanga na Goran Kopunovic wa Simba kwa kutangazwa kuwa Kocha Bora wa msimu uliopita.Mmoja wa wadau waliopinga tuzo ya Makata na Kado aliyewazidi Said Mohammed wa Mtibwa Sugar na Mohammed Yusuph wa Prisons, ni Hafidh Saleh, meneja wa Yanga.

Hafidh alisema: “Hivi inaingia akilini kocha kuchukua tuzo kwa mechi nane? Hata Kado mwenyewe hajacheza muda mrefu pale Coastal Union, muda mrefu alikuwa nje akiuguza mkono, ila kwa Msuva haina tatizo.”

Kwa upande wake, Ofisa Habari wa Ruvu Shooting iliyoshuka daraja, Masau Bwire, alisema: “Sina tatizo na tuzo nyingine, ila ninatatizika sana na tuzo ya kocha na kipa bora, hakuna asiyejua soka la Tanzania mechi za mwishomwisho zinakuwa na vitu vingi.

“Huwezi kumlinganisha na makocha waliongia kwenye kinyang’ayiro kile. Kwa Kado kuwa kipa bora! Bora nisiongee maana ninaweza kuzungumza mengi ya kuniweka pabaya.” Hata hivyo, Makata alijipigia debe kwa kusema kuwa alistahili kwani kuibakiza timu katika ligi haikuwa kazi ndogo kama wengi wanavyodhani.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.