Baadhi ya raia ya kigeni wakiwa wamehifadhiwa katika kambi baada ya kukimbia fujo na kuepusha maisha yao.
Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini
umesema umeanza utambuzi wa Watanzania waishio katika maeneo ya hatari
nchini humo kabla ya kuanza hatua za kuwaondoa na kuwarejesha nyumbani.
Hatua hiyo inatokana na kushamiri kwa
mashambulizi yanayofanywa na raia wa Afrika Kusini dhidi ya raia wa
kigeni ambapo hadi kufikia jana watu sita wameuawa.
Taarifa zilizopo hata hivyo zinasema
kwamba hakuna raia wa Tanzania ambaye ameuawa au kujeruhiwa katika
vurumai hizo ambazo zimeanza Durban, Kwa- Zulu Natal.
Mkuu wa Mawasiliano, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mindi Kasiga, amesema kwamba Ubalozi Afrika Kusini umepeleka maofisa wake katika mji wa Durban kuangalia hali ilivyo.
Kasiga amesema kwamba serikali imeshatoa mwongozo wa namna ya kuwaondoa raia wake nchini Afrika Kusini.
“Utaratibu
wa kuwaondoa Watanzania upo tayari, lakini itambulike kwamba si kila
Mtanzania anayeishi Afrika Kusini ataondolewa bali wale walio katika
maeneo hatarishi.
“Tutawaondoa
Watanzania ambao wanaishi katika mazingira yaliyotishio au wale ambao
mali zao zimeharibiwa,” alisema Kasiga akizungumza na gazeti dada Daily
News kwa njia ya simu jana.
Alisema kwamba Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, ambaye yuko nje kwa safari ya kikazi atatoa taarifa mara tu atakapowasili nchini.
“Kwa sasa waziri yupo nchini Jordan lakini atakuwa na nafasi ya kuzungumzia suala hili mara tu atakaporejea siku chache zijazo,” Kasiga.
-HABARILEO

Note: Only a member of this blog may post a comment.