Waziri Mkuu Mteule wa Tanzania, Kassim Majaliwa
Hilo ndiyo neno pekee unaloweza
kulitumia kueleza uteuzi wa Kassim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu wa
Tanzania, uliofanywa na Rais wa Awamu ya Tano wa Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, jana, Novemba 19, 2015
kisha kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Majaliwa alipitishwa kwa kura 258 kati
ya 349 zilizopigwa ukiwa ni ushindi wa asilimia 73.5 ambapo waandishi
wetu waliokuwa bungeni mjini Dodoma na Dar es Salaam, walikuwa makini
kufuatilia kila kilichokuwa kinaendelea na hapa wanakuletea ripoti
kamili:
HAKUTARAJIWA NA WENGI
Jina la Majaliwa, halikuwa miongoni mwa
majina ya wanasiasa kadhaa waliokuwa wakitajwa mara kwa mara, hasa
kwenye vyombo vya habari kwamba wanaweza kutwaa nafasi hiyo.
Miongoni mwa wanasiasawaliokuwa
wakipigiwa sana chapuo kwamba wanaweza kuvaa viatu vya uwaziri mkuu
kutokana na utendaji wao wa kazi na majina ya majimbo wanayoyaongoza
kwenye mabano, ni pamoja na Dk. Harrison Mwakyembe (Kyela), William
Lukuvi (Ismani), January Makamba (Bumbuli), Prof. Sospeter Muhongo
(Musoma Vijijini), Mwigulu Nchemba (Iramba Magharibi) na wengine wengi.
UPEPO WABADILIKA GHAFLA
Hata hivyo, siku moja kabla ya mchakato
wa uteuzi wa waziri mkuu, upepo wa kisiasa ulibadilika baada ya majina
mawili kuvuja kutoka vyanzo vya ndani vya serikali; Ramo Makani, Mbunge
wa Tunduru Kaskazini, alikuwa akipewa nafasi kubwa huku Majaliwa,
akimfuatia kwa sifa za kuukwaa wadhifa huo nyeti serikalini.
Hata hivyo, mambo yaliendelea kuwa
tofauti ambapo kwa mujibu wchanzo chetu cha ndani, jina la Makani
lilikatwa kwa kigezo kwamba hakuwa na uwezo wa kuongoza baraza la
mawaziri kwa sababu hakuwahi kuwa waziri hivyo kukosa uzoefu.
Bahati ya mtende ikamuangukia Majaliwa
ambaye kabla ya jana kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu, alikuwa Naibu Waziri wa
Nchi, Ofisi ya WaziriMkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi) akishughulika na upande wa elimu, nafasi aliyoitumikia kwa
muda wa miaka mitano, tangu alipoteuliwa na Rais (mstaafu), Jakaya
Mrisho Kikwete, mwaka 2010.
USIRI MKUBWA WATAWALA
Usiri mkubwa ulitawala katika mchakato
wa kumtangaza waziri mkuu, ambapo tofauti na miaka mingine yote ambapo
spika wa bunge ndiye hulifuata jina la waziri mkuu mteule kwa mheshimiwa
rais, jana alimtuma Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila kufuatilia
jina hilo kwa Mhe. Magufuli lakini ikashindikana.
Badala yake, tofauti kabisa na utaratibu
wa miaka yote, Rais Magufuli alimtuma mlinzi wake wa karibukulipeleka
jina hilo bungeni, akaingia akiwa na bahasha huku akisindikizwa na
askari wa bunge na kwenda kumkabidhi Spika wa Bunge, Job Ndugai.
Kingine kilichomshangaza spika ni kukuta
ndani ya bahasha hiyo kuna bahasha nyingine mbili ambazo zote zilikuwa
zimefungwa kwa gundi maalum ambapo alizifungua moja baada ya nyingine na
hatimaye kukutana na jina la waziri mkuu.
Ajabu nyingine ni kwamba taarifa ya rais
kwenda kwa spika, kuhusu kumteua Majaliwa ilikuwa imeandikwa kwa mkono
na rais mwenyewe, tofauti na miaka yote ambayo huchapwa kwa mashine.
Baada ya yote, Spika Ndugai aliusoma
ujumbe huo na alipolitaja jina la mbunge huyo wa Ruangwa, mshangao na
mshtuko vilionekana Dhahiri miongoni mwa wabunge kwani ni jambo ambalo
halikutarajiwa na wengi.
WENGINE WAONESHA WASIWASI WAO
Baada ya jina hilo kutajwa, baadhi ya
wabunge walionesha dhahiri wasiwasi wao kama Majaliwa anaweza kumudu
kushika wadhifa huo mkubwa serikalini, hasa ikizingatiwa kwamba hakuwahi
kufikia ngazi ya uwazirikamili zaidi ya kukomea kwenye unaibu.
“Uwaziri mkuu siyo kazi lelemama,
mheshimiwa hajawahi kuwa waziri kamili, anawezaje kuongoza baraza la
mawaziri?” alinukuliwa mheshimiwa mmoja aliyeomba hifadhi ya jina lake.
Hata hivyo, wasiwasi huo ulipingwa na baadhi ya waheshimiwa wengine
waliomtolea mfano Mhe. Frederick Sumaye kwamba naye wakati anateuliwa
kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin William
Mkapa, alikuwa Naibu Waziri wa Kilimo lakini akavunja rekodi ya kuwa
waziri mkuu pekee aliyeshika wadhifa huo kwa kipindi chote cha miaka
kumi.
NI WA PILI KUTOKA TAMISEMI
Ukiachilia mbali Majaliwa aliyetokea
Tamisemi, waziri mkuu aliyemaliza muda wake, Mizengo Pinda naye alitokea
kwenye wizara hiyohiyo, hivyo kufanya mpaka sasa wizara hiyo kutoa
mawaziri wakuu wawili mfululizo, jambo ambalo halijawahi kutokea kwenye
wizara nyingine yoyote.
RUANGWA CHEREKOCHEREKO
Mwandishi wetu aliyekuwa jimboni kwa
Mhe. Majaliwa wakati jina lake likitangazwa kuwa waziri mkuu, anaeleza
kwamba maeneo mbalimbali ya jimbo hilo, ikiwa ni pamoja na kijiji
alichozaliwa cha Mnacho, yalitawaliwa na cherekochereko ambapo wananchi
wengi walikuwa wakiimba nyimbo za furaha na kumpongeza mbunge wao kwa
kuteuliwa kushika nafasi hiyo kubwa serikalini.
KUBENEA, MBATIA WAPINGA KUMPIGIA MAKOFI MAJALIWA
Wakati wa shamrashamra za kumpongeza
Majaliwa bungeni baada ya jina lake kutangazwa, tafrani kidogo iliibuka
baada ya Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola kuwataja Mbunge wa Ubungo, Saed
Kubenea na Mbunge wa Vunjo, James Mbatia kwamba aliwaona wakipiga
makofi wakati jina la Majaliwa likitangazwa, jambo ambalo wawili hao
walilipinga vikali na kusababisha mvutano ndani ya bunge wakimtaka afute
kauli yake, jambo ambalo baadaye alilifanya baada ya spika kuingilia
kati.
NI MCHAPAKAZI KAMA MAGUFULI
Watu waliowahi kufanya kazi na Majaliwa,
wanamueleza waziri mkuu huyo mteule kwamba anaweza kuendana na kasi ya
Rais Magufuli kwa sababu naye ni mchapakazi, asiyependa kukaa ofisini na
kusubiri ripoti.
“Alipokuwa Tamisemi, alitembelea karibu
nchi nzima kutafuta matatizo yaliyokuwa yanaikabili wizara yake, akawa
anazungumza na walimu na watumishi wengine wa serikali na kusikiliza
matatizo yao jambo ambalo hata Magufuli analo,” mtumishi mmoja wa wizara
hiyo, alilitonya Uwazi Mizengwe kwa masharti ya kutotajwa jina lake.
WABUNGE WANAMZUNGUMZIAJE MAJALIWA
Baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, wamemzungumzia kwa urefu Waziri Mkuu mteule wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa ambapo
walisema:
EZEKIEL MAIGE (MSALALA)
“Kwanza ni kijana ambaye kwa hakika
ataendana sawa na falsafa ya Rais Dk. Magufuli ya ‘Hapa Kazi Tu’. Lakini
pia Majaliwa ni mchapakazi tena mfuatiliaji
wa mambo kwa vitendo, kwa hiyo ni chaguo sahihi.”
IBRAHIM RAZAZ (KIEMBESAMAKI)
“Majaliwa hana makundi, si mtu wa kupokea majungu, hivyo tutarajie utendaji usiokuwa na msukumo wa nguvu ya watu wachache.”
WILLIAM LUKUVI (ISMANI)
“Ni mtu msikivu, muadilifu, hana makundi lakini pia ni mtu wa bidii, ….nimpongeze Mhe. Rais kwa kutuchagulia mtu sahihi.”
MBONI MHITA (HANDENI VIJIJINI)
“Ni mzoefu katika utendaji, mkimya
lakini mfuatiliaji wa mambo kwa vitendo na si kwa maneno mengi na
makelele, pia ni muadilifu.”
MAGDALENA SAKAYA (KALIUA)
“Hana kashfa, mimi namfahamu vyema kwa
sababu alikuwa mkuu wangu wa wilaya kule Urambo, hata alipoacha nafasi
hiyo na kwenda kugombea ubunge huko Ruangwa, nakumbuka wananchi wa
wilaya ya Urambo walisikitika sana.”
PETER MSIGWA (IRINGA MJINI)
“Binafsi sijaridhika na uteuzi huu,
kwanza kwa sasa kama nchi, tunahitaji waziri mkuu mtendaji na mwenye
kufanya uamuzi kwa wepesi, sasa kwa haiba ya Majaliwa, sioni hali hiyo,
mimi ni jamaa yangu kabisa, lakini sidhani kama anaweza kukikalia kiti
hicho.”
DAVID SILINDE (MOMBA)
“Kwanza imekuwa tofauti kabisa na
matarajio ya wengi, kwamba kila mtu alikuwa na hisia ya watu wengine
maarufu sana wa siasa, lakini hali imekuwa nyingine, Mjaliwa si mtu wa
kujikweza hata kwake anaishi maisha ya kawaida kabisa, ni mtulivu,
naamini ni chaguo sahihi.”
KHAMIS KINGWALA (NZEGA VIJIJINI)
“Kusema kweli Majaliwa ni mtu mwenye
hekima na busara za hali ya juu, nimefanya naye kazi kwa maeneo mengi,
hata kwenye upande wa michezo amekuwa mwalimu wetu wa timu ya Bunge
Sports Club; namjua.”
KANGI LUGOLA (MWIBARA)
“Hakutarajiwa, lakini ni mtu makini sana
hususan kwa viongozi wazembe, mfano mzuri ni kule jimboni kwangu kuna
shule moja walimu walifanyiwa mchezo wa kishirikiana, nilipompelekea
shauri hilo, ni yeye ndiye alikuwa akinipigia simu na wakati mwingine
usiku wa manane, akitaka kujua maendeleo ya walimu hao, kwa hiyo ni mtu
mfuatiliaji.”
Note: Only a member of this blog may post a comment.