
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Maxmillan Lyimo, amesema akipata ridhaa ya kuwaongoza Watanzania katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, atahakikisha makundi yote ya jamii yanapewa mikopo ambayo itafuta machungu ya ukosefu wa ajira.
Lyimo atoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wakazi wa Mwika, Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro, ikiwa ni siku ya tano, tangu TLP ilipozindua kampeni za mgombea urais wa chama hicho.
“Nataka nimalize kabisa tatizo la ajira ambalo linatesa nchi yetu kwa miaka 52 sasa; mkinipa ridhaa ya kuunda serikali ya awamu ya tano, nitaweka utaratibu wa kuyawezesha makundi yote kupata mikopo, kuanzia ngazi ya vijiji, sera hii inatekelezeka kwangu na siyo CCM inayowadanganya itawapa milioni 50,”alisema mgombea huyo.
Alisema katika suala la elimu, atafanya mabadiliko makubwa, kwa kufuta mfumo wa kibaguzi uliopo hivi sasa ambao unatoa fursa ya kuwagawa Watanzania kwa makundi ya watoto wa matajiri na masikini, katika kupata elimu bora.
Lyimo ni miongoni mwa wagombea wanane ambao wamejitokeza kuwania nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Wagombea wengine wa kiti hicho ni Dk. John Magufuli (CCM), Anna Mgwira (ACT-Wazalendo), Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowasa ambaye anapeperusha bendera ya vyama vinavyounda Ukawa, kupitia Chadema; Chief Lutalosa Yemba (ADC), Janken Kasambala (N.R.A) na Hashim Rungwe (Chaumma).
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Taifa wa TLP na mgombea ubunge wa Jimbo la Vunjo, Augustino Mrema, alirejea kauli yake ya muda mrefu kwamba, bado ana nguvu ya kushughulikia changamoto na kero za jimbo hilo, hivyo ana kila sababu ya kuchaguliwa ili azitafutie ufumbuzi wa kudumu.
“Mimi nazijua siasa za upinzani, kuliko mtu mwingine yeyote na ndio maana wananiogopa wakisema eti mimi ni CCM ‘B’ sasa hebu rudisheni mioyo yenu mkanichague ili niendelee kusaidia miradi ya maendeleo pamoja na kutatua kero zinazowakabili wananchi wangu,"alisema Mrema.
Chanzo: NIPASHE

Note: Only a member of this blog may post a comment.