Kuna mambo mengine mtu unafanya kisha yanageuka maana na kukuweka katika hali ya sintofahamu. Lakini lililonikuta juzi mpaka sasa nacheka huku nalia peke yangu hata usiku wa manane. Unajua kama wiki tatu zilizopita yule mchumba wangu niliyewatambulisha kwenu si kaamua kuniacha baada ya kukutana na jamaa mmoja mwongo wa kutisha.
Mchumba wangu ameona hiyo ni fursa ya wazi ya kuwa na mkwe rais na kaniacha kwa vimbwanga ambavyo bado vinaniuma. Mchumba wangu siku hizi ni kada wa nguvu, anampigia debe baba mkwe mtarajiwa. Kwenye mambo haya ya siasa watu tuna sababu mbalimbali za ajabu sana kwa nini unamtaka huyu awe rais na kwa nini humtaki yule mwingine.
Juzi katika pitatapita yangu nikawa kwenye uwanja wa kuegesha magari wa maduka maarufu, hapa ni kitovu cha wadada bomba kufika wakiwa katika mipango yao ya kununua vitu mbalimbali. Kama kawaida nikiwa katika tathmini ya mchumba bomba, kwa mbali akatokea binti mmoja akiwa anaelekea kwangu, aise yaani roho yangu ikashtuka.
Sijawahi kuona binti kaumbika kama yule, palepale nikaamua huyu ndiye niliyekuwa namtafuta. Akawa anaelekea nilikokuwa, akatabasamu, ilikuwa kama kwenye sinema, mambo yote yalikuwa slow moshen, akanyanyua mkono kunipungia, nami nikanyanyua mkono na kumpungia, huku kimoyomoyo nikishukuru Mungu kwa kunichagulia kiumbe kama huyu kuwa wangu wa maisha tena bila mimi kusema hata neno moja.
Tukasogeleana tukipungiana mikono, tulipokaribiana kama hatua kumi, nikashangaa, kumbe alikuwa anampungia mkono mtu aliyekuwa nyuma yangu, tulipopishana nikabaki mkono hewani, sikujua niushushe au ubaki juu. Nikauteremesha taratibu na kujidai nilikuwa najikuna kichwa. Machozi yakanilengalenga.
Note: Only a member of this blog may post a comment.