KUFUTWA
KWA KIBALI KILICHOANZISHA VYUO VIKUU VISHIRIKI VYA SAYANSI ZA KILIMO NA
TEKNOLOJIA (SJUCAST) NA TEKNOLOJIA YA HABARI (SJUCIT) VYA CHUO KIKUU
CHA MT. YOSEFU TANZANIA (SJUIT), KAMPASI YA SONGEA
1. Tunapenda
kuuarifu umma kwamba, Chuo Kikuu cha Mt. Yosefu Tanzania (SJUIT) ni
mojawapo ya vyuo vikuu vilivyosajiliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania
(TCU). Chuo hiki kinamilikiwa na Shirika la Kitawa la Dada wa Maria
Imakulata (DMI) pamoja na washirika wao. Hapa nchini chuo hiki
kilianzishwa mwaka 2003 chini ya usajili wa Baraza la Taifa la Elimu ya
Ufundi (NACTE). Mnamo mwaka 2011, chuo hiki kiliwasilisha maombi ya
kusajiliwa na TCU. Maombi hayo yaliidhinishwa na Tume tarehe 14 Desemba,
2011. Kisha tarehe 27 Septemba, 2012 kufuatia maombi ya uongozi wa
Chuo, Tume iliidhinisha kuanzishwa kwa Vyuo Vikuu Vishiriki vitatu
ambavyo ni: Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi za Kilimo na Teknolojia (St. Joseph University College of Agricultural Science and Technology - SJUCAST), na Chuo Kikuu Kishiriki cha Teknolojia ya Habari (St. Joseph University College of Information Technology - SJUCIT) ambavyo vilianzishwa Songea; na Chuo Kikuu Kishiriki cha Uongozi, Uhasibu na Fedha (St. Joseph College of Management, Accounting and Finance - SJUCMAF)
kilichopo Makambako, Njombe. Hivi sasa Chuo Kikuu hiki kina Kampasi
nyingine Arusha, Boko na Luguruni, Dar es Salaam, huku Makao Makuu
yakiwa katika Kampasi ya Luguruni.
2. Kwa
mujibu wa kifungu cha 5(1) cha Sheria ya Vyuo Vikuu, Sura ya 346 ya
Sheria za Tanzania, Tume ina mamlaka ya kusimamia na kudhibiti ubora na
usimamizi wa uendeshaji wa Vyuo Vikuu hapa nchini.
3. Kwa
muda mrefu katika Vyuo Vikuu Vishiriki vya Sayansi za Kilimo na
Teknolojia (SJUCAST) na Teknolojia ya Habari (SJUCIT) kumekuwapo na
mlolongo wa matatizo ya ubora, uongozi, ukiukwaji wa sheria na taratibu
za uendeshaji wa chuo kikuu kama zilivyobainishwa na Sheria ya Vyuo
Vikuu. Jitihada za Tume ya Vyuo Vikuu kukitaka Chuo Kikuu cha Mt. Yosefu
Tanzania (SJUIT) kuhakikisha hivi Vyuo Vikuu Vishiriki vinatoa elimu
inayokidhi viwango vya ubora vilivyowekwa na Tume hazikupewa uzito
stahiki na uongozi wa chuo. Matokeo yake wanafunzi wa SJUCAST na SJUCIT
wamekuwa hawapati elimu kwa kiwango stahiki. Hivi sasa katika vyuo hivi
vishiriki viwili kuna jumla ya wanafunzi 2046 wanaosoma programu za
digrii zifuatazo:
a)Bachelor of Technology in Agriculture [B. Tech. in Agriculture](wanafunzi 282)
b)Bachelor of Technology in Horticulture [B. Tech. in Horticulture](wanafunzi 61)
c)Bachelor of Technology in Agricultural Engineering [B. Tech. in Agric. Eng.]
(wanafunzi 255)
d)Bachelor of Technology in Food Process Engineering [B. Tech. in FPE.]
(wanafunzi 238)
e)Bachelor of Science with Education (wanafunzi 732)
f)Bachelor of Science in Computer Science (wanafunzi 250)
g)Bachelor of Computer Science with Education and Bachelor of Science in
Education with Computer Science (wanafunzi 196)
h)Diploma in Computer Science (wanafunzi 81)
4.Kutokana
na yaliyobainishwa hapo awali, tunapenda kuuarifu umma kwamba, Tume
imejiridhisha kuwa hivi Vyuo Vikuu Vishiriki viwili havitoi elimu ya
chuo kikuu ya viwango stahiki. Kwa kuzingatia ukweli kwamba wanafunzi
katika vyuo hivi vishiriki vya SJUCAST na SJUCIT ndio waathirika wakuu
wa matatizo yaliyopo kwenye vyuo hivi, Tume imeamua kufuta kibali kilichoanzisha hivi vyuo vikuu vishiriki viwili yaani: St. Joseph University College of Agricultural Science and Technology (SJUCAST) na St. Joseph University College of Information Technology (SJUCIT); na kuidhinisha uhamisho wa wanafunzi wote waliokuwa wanasoma katika vyuo hivyo kwa gharama za Chuo Kikuu cha SJUIT.
Uhamisho huo pia unahusu wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wa pili wanaosoma digrii za Bachelor of Technology in Agricultural Engineering [B. Tech. in Agric. Eng.] na Bachelor of Technology in Food Process Engineering [B. Tech. in FPE.] ambao hivi sasa wanasoma katika Kampasi ya Luguruni, Dar es Salaam.
5. Kufuatia
uamuzi huu, wanafunzi wote wanaosoma katika Vyuo Vikuu vishiriki vya
SJUCAST na SJUCIT wanaarifiwa kuwa watahamishiwa kwenye vyuo vikuu
vingine vinavyofundisha programu za masomo zinazofanana na masomo
wanayosoma hivi sasa chini ya utaratibu na masharti yafuatayo:
i) Wanafunzi
wote wanapaswa kuondoka chuoni mara moja baada ya kukamilisha taratibu
za kukabidhi mali na vifaa vingine vya chuo kwa mujibu wa taratibu
zilizowekwa.
ii)Wanafunzi
wote wanatakiwa kuripoti kwenye vyuo watavyopangiwa wakati wa
kufunguliwa kwa muhula (semester) wa pili. Tarehe halisi ya kuanza kwa
muhula wa pili kwa kila chuo watakachopangiwa itatangazwa na kuwekwa
kwenye tovuti ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania.
iii)Wanafunzi wote wanaosoma digrii ya sayansi za kilimo na uhandisi(programmes related to agricultural sciences and engineering)watahamishiwa katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
iv)Wanafunzi
wanaosoma digrii ya ualimu wa sayansi watahamishiwa katika mojawapo ya
vyuo vikuu vifutavyo: Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
(SUA); Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM); na Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mwenge (MWECAU).
v)Wanafunzi
wote wanaosoma digrii na diploma ya sayansi ya kompyuta watahamishiwa
katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA). vi) Wanafunzi wote
wanaosoma digrii ya ualimu na sayansi ya kompyuta watahamishiwa katika
Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Ruaha (RUCU).
vii)Orodha
ya wanafunzi waliohamishwa na majina ya vyuo vikuu walivyohamishiwa
itatangazwa na kuwekwa kwenye tovuti ya Tume ya Vyuo Vikuu hivi punde.
viii)Wanafunzi
wote waliohamishwa ambao hawakukamilisha mitihani yao ya mwisho wa
muhula wa kwanza, au hawakufanya kabisa mitihani hiyo, watatakiwa
kufanya mitihani hiyo katika vyuo vikuu watavyohamishiwa kwa utaratibu
maalum utakaondaliwa na chuo husika.
ix)Kila
mwanafunzi anawajibika kutunza kumbukumbu zake zote muhimu za maendeleo
ya kitaaluma kwa ajili ya matumizi ya baadaye, ikiwa ni pamoja na
matokeo ya mitihani aliyokwishafanya.
x)Wanafunzi
wote ambao ni wanufaika wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu,
mikopo yao itahamishiwa katika vyuo wakapokuwa wamehamishiwa.
6.Kampasi nyingine za Chuo Kikuu cha SJUIT zinaendelea na masomo kama kawaida.
7.Kwa
taarifa hii, vyuo vikuu vyote nchini vinakumbushwa kufuata sheria na
kuzingatia utoaji wa elimu inayokidhi viwango vya ubora vinavyokubalika
kitaifa na kimataifa. Tume haitasita kuchukua hatua stahiki kwa chuo
kikuu chochote kitakachobainika kutoa elimu isiyokidhi viwango vya ubora
kwa kisingizio cha aina yoyote.
Imetolewa na
PROF. YUNUS D. MGAYA
Katibu Mtendaji
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania
19 Februari 2016


Note: Only a member of this blog may post a comment.