Brighton Masalu
SIKU chache baada ya kushinda kesi ya tuhuma za kubaka iliyokuwa
ikimkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam,
mwimbaji wa muziki wa Injili, Emmanuel Mbasha anatarajiwa kupandishwa
tena katika korti hiyohiyo kwa madai mengine, Risasi Mchanganyiko lina
habari kamili.
Mwimbaji wa muziki wa Injili, Emmanuel Mbasha.
Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni kwa sharti la kutotajwa
jina, mmoja wa watu wa karibu na wanandoa hao, alisema Flora amefungua
kesi ya madai ya talaka katika Mahakama ya Kisutu na kwamba muda si
mrefu shauri hilo litaanza kusikilizwa.
“Flora ameenda mahakamani kudai talaka yake, kwa hiyo kesi
inatarajiwa kuanza kusikilizwa muda wowote kuanzia sasa,” alisema mtoa
habari huyo.Baada ya taarifa hizo, mwandishi wetu alimtafuta Mbasha kwa
njia ya simu na kumuuliza juu ya madai hayo, ambapo alikiri na kudai
anajiandaa kukabiliana na shitaka hilo.
“Yeah, ni kweli kaka, Flora ameamua kwenda mahakamani kudai talaka
yake, sioni kama ni tatizo, kwa sasa siwezi kuzungumza lolote kwa sababu
limeshafika katika mkondo wa sheria na tunapaswa kusubiri tuone
kitakachotokea, lakini naamini kila kitu kitakwenda sawa,” alisema
Mbasha.
Kwa upande wake, mke wa mwimbaji huyo, ambaye pia ni mkali wa nyimbo
za gospo, Flora Mbasha alipotafutwa hakupokea simu yake ya mkononi,
lakini alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno (sms) alijibu kwa kifupi:
“Kaka, naendesha, kila kitu kiko mahakamani kwa hiyo sina la kuzungumza kwa sasa.”
Kwa muda mrefu, waimbaji hao wamekuwa katika mgogoro wa kifamilia ambapo juhudi za watu mbalimbali zimefanyika kusuluhisha lakini hazikufanikiwa.
Note: Only a member of this blog may post a comment.