









XIONG SHUIHUA (54) ambaye alizaliwa
katika kijiji kiitwacho Xiongken, kusini mwa China, hivi karibuni
aliamua kukijenga upya kijiji alichozaliwa na kukulia kama shukurani kwa
wakazi wake ambao alikuwa nao wakati wa nyakati ngumu za umaskini,
kabla hajapata utajiri.
Mtu huyo ambaye sasa ni milionea
kutokana na biashara ya viwanda vya chuma, aliamua kurejea katika
kijiji chake hicho cha nyumbani kwao ambako kulikuwa na vibanda na
nyumba chafu walizokuwa wanaishi wanakijiji wake.
Njia za kijiji hicho zilikuwa zimejaa
uchafu na marundo ya taka kila mahali. Hivyo Xiong alipoyaona yote hayo
aliamua kuyabadili maisha ya wakazi wa kijiji hicho.
“Nilipata fedha nyingi ambayo
nikashindwa kufahamu nitaitumiaje, hivyo nikakumbuka nilikotoka,
nikaamua kuwasaidia watu wote walionisaidia mimi na familia yangu
nilipokuwa mdogo,” anasimulia.
Hivyo, alivibomoa vibanda vyote na
kujenga maghorofa ya kisasa na akajenga barabara mpya sehemu zilizokuwa
na njia chafu na kulifanya eneo hilo kuwa la kisasa.
Isitoshe, milionea huyo mkaribu akamua kuwapa wazee na familia zenye vipato vya chini, milo mitatu ya bure kila siku.
Kutokana na ukarimu huo, hivi sasa
familia 72 zinaishi katika nyumba za kisasa na familia zingine 18
ambazo zilimsaidia sana, zilijengewa nyumba mpya, kubwa kila moja ikiwa
ni baada ya kuishi katika mabanda ya miti kwa miaka nenda-rudi.
Mzee mmoja aitwaye Qiong Chu (75)
alisema: “Nakumbuka wazazi wa Xiong walikuwa ni wakarimu kwa watu wote,
ni jambo jema kwamba mtoto wao amerithi ukarimu huo.”
Note: Only a member of this blog may post a comment.