Monday, September 7, 2015

Anonymous

CANNAVARO Awacharukia Mastraika Timu ya Taifa, MKWASA Amtuliza!

Nahodha wa Taifa Stars, Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Mohammed Mdose, Dar es Salaam
NAHODHA wa Taifa Stars, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, amesema kuwa kama washambuliaji wa Stars wangekuwa makini basi wangeweza kuwafunga Nigeria lakini kocha wao Charles Boniface Mkwasa, amesema hali hiyo ni ya kawaida.

Stars na Nigeria zilikutana juzi Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kwenye mchezo wa kufuzu Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) 2017 nchini Gabon na kumaliza dakika 90 bila kufungana, licha ya Stars kuutawala mchezo na kukosa nafasi kadhaa za wazi za kufunga.
Wachezaji wa Stars, Thomas Ulimwengu na Mrisho Ngassa walipata nafasi za kufunga lakini mipira yao haikuwa na macho ya kupenya langoni mwa Nigeria.

Cannavaro alisema Stars ilijitahidi kuikamata Nigeria kila idara na walikuwa na uwezo wa kuwafanya watakavyo lakini walikwama katika kukwamisha mipira wavuni.
“Siwezi kumtaja mmojammoja lakini tulichoshindwa ni kufunga mabao lakini tuliwamudu kila idara, kama tungekuwa makini basi tungewafunga, nafasi bado tunayo kujirekebisha katika mechi zijazo,” alisema Cannavaro.

Kwa upande wa Mkwasa, alisema kuwa kukosa mabao ya wazi kama walivyofanya washambuliaji wake ni tatizo kubwa lakini akagoma kutupa lawama kwa mchezaji yeyote, badala yake akasisitiza atafanya kila awezalo kulimaliza tatizo hilo.
“Siyo muda wa kuanza kumlaumu mmojammoja ila cha kufanya ni kulifanyia kazi tatizo kuona hatufanyi tena kosa hili ambalo limetugharimu kwenye mchezo ambao tulikuwa na uwezo wa kushinda,” alisema Mkwasa.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.