BONGO ni vilio! Kufuatia Watanzania wanne mahujaji miongoni mwa 717
waliopoteza maisha kwa kukanyagana mjini Mina, Maka, Saudi Arabia, hapa
Bongo vilio vinaendelea hasa kufuatia habari kuwa, miili ya marehemu hao
haitarudishwa nyumbani kwa mazishi.
Marehemu, Seif Salim Kitimla enzi za uhai wake.
Tukio la mahujaji hao kupoteza maisha lilijiri Alhamisi iliyopita
wakati wa zoezi la kumpiga mawe shetani ikiwa ni sehemu ya nguzo kuu
katika ibada ya hija kila mwaka nchini humo.Watanzania ambao mpaka sasa
wamethibitishwa kupoteza maisha ni Mwanaisha Hassan Juma, Mkungwe
Suleiman Hemed na Seif Salim Kitimla.
Mwanamke mwingine Mtanzania jina halijapatikana. Pia kuna raia mmoja
wa Kenya, Fatuma Mohammed Jama ambaye alikwenda Maka kwa kutokea nchini.
Jijini Dar, Gazeti la Uwazi baada ya kupata taarifa hizo liliingia
mtaani ili kupata nyumba zenye misiba kwa lengo la kuzungumza na wafiwa
na kufanikiwa kufika katika msiba wa mmoja wa marehemu, Seif Salim
Kitimla (59) ambapo hitima ya kumuombea ilifanyika nyumbani kwake Mtaa
wa Chekeni Kijiji cha Mwasonga wilayani Temeke, Dar, Jumamosi iliyopita.
MTOTO WA MAREHEMU
Akizungumza na Uwazi Jumamosi iliyopita, mtoto wa tatu kati ya kumi
wa marehemu Seif, Sinani Seif Kitimla alisema kifo cha baba yao
kimewasikitisha sana na kwa mara ya kwanza hawakuamini kama amefariki
dunia maana familia ilipata jina tofauti na walipofuatilia ndipo
wakapata taarifa sahihi.
Mke wa marehemu Seif.
“Tangu baba ameondoka kwenda hija nilikuwa nikiwasiliana naye mara
kwa mara. Mara ya mwisho tuliwasiliana Jumatano (iliyopita) jioni,
nikampa taarifa ya huku nyumbani.”“Baada ya mazungumzo akaniambia kuwa,
siku ya Alhamisi na Ijumaa hatakuwa hewani na simu ataiacha hotelini.
“Alinieleza hivyo kwa sababu siku hizo mbili ndiyo walikuwa wakienda
huko (kumpiga mawe shetani). Lakini Ijumaa nilimpigia simu hakupatikana.
Hapo tulishasikia habari zilizotokea huko na kupata jina lenye
mkanganyiko.
“Ilibidi niende kazini kwake, Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
Tawi la Bandari kuulizia kama wana taarifa yoyote pia kuhakikisha jina.
“Kule nao walisema hakuna lolote ingawa walisema kama ni kweli ni
pigo kwao. Baadaye tulikuja kuhakikisha kwa kufanya mawasiliano na Ofisi
za Baraza Kuu la Waislam Tanzania (Bakwata) na Ofisi za Ubalozi wa
Saudi Arabia ndiyo tukapata uhakika kwamba ni baba. Leo tumefanya sala
na kila mmoja atatawanyika hapa, maana wanasema watazika hukohuko,”
alisema mtoto huyo.
Mufti Zuberi.
Msiba mwingine wa Mwanaisha ulitajwa kuwa Buguruni, Dar lakini Uwazi
lilipofika eneo hilo taarifa zilisema hakuna msiba kwa vile mwili wa
marehemu hautarejeshwa nchini.
MAHUJAJI WALIOSALIMIKA
Ukiachia Watanzania hao kupoteza maisha, Bakwata imesema Watanzania
wengine wapo salama na habari zaidi zitatolewa baadaye.Kwa mujibu wa
Uwazi, Watanzania walionusurika wamo mchekeshaji maarufu nchini, Athuman
Amiri ‘Mzee Majuto’, aliyekuwa Mbunge wa Tabora Mjini kwa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Ismail Aden Rage, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha
Wananchi (Cuf), Ibrahim Lipumba na mchezaji wa zamani wa Timu ya Yanga,
Sunday Manara.
Wengine ni mfanyakazi wa Shirika la Ugavi Tanzania (Tanesco), Fatuma
Korongo, Mufti Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zuberi, Shehe wa Mkoa wa Dar
es Salaam, Alhadi Musa Salum, Shehe Musa Kundecha na wengine ambao
majina hayakupatikana.
Serikali ya Saudi Arabia hutumia zaidi ya Dola Bilioni 60 kila mwaka
kuimarisha miundombinu ya shughuli hiyo kama ukarabati wa misikiti. Pia,
mambo ya kiusalama huimarishwa ambapo zaidi ya kamera za CCTV 5000
huwekwa kama tahadhari kwani zaidi ya mahujaji milioni 2 wanatajwa
kuhudhuria shughuli hiyo takatifu ya kila mwaka.
Mina ni kitongoji chenye ukubwa wa eneo la mraba wa kilometa 20
katika eneo liitwalo Jamaraat. Kiimani eneo hilo ndipo mahujaji hurusha
mawe kama ishara ya kuenzi kile ambacho Nabii Ibrahim alikifanya
alipotokewa na mwovu shetani.
Hadi sasa inakadiriwa kuwa, zaidi ya watu 3,929 wamekwishafariki
dunia kwa sababu mbalimbali huko Mina kwenye shughuli ya hija ikiwemo
joto, kuangukiwa na ukuta, misongamano, moto kuunguza mahema na
kukanyagana.
Miaka na idadi ya watu waliofariki dunia kwenye mabano ni kama
ifuatavyo: Mwaka 1987 (400), 1990 (1400), 1994 (270), 1997 (350), 1998
(180), 2001 (35), 2004, (250), 2006 (362) kabla ya safari hii.
Waombolezaji wakiwa msibani.
Msemaji mmoja wa balozi ndogo ya Tanzania iliyopo mjini Mina alisema
kukanyagana kwa mahujaji safari hii kulitokana kuachwa kwa utaratibu wa
awali ambapo mahujaji huenda kumpiga shetani kwa awamu, lakini safari
hii walikwenda kwa pamoja.
Ziko habari kuwa, ni utaratibu wa kiimani, mahujaji wanapofia Maka
ambao ni mji mtakatifu huzikwa eneo hilohilo kwa maana ya kupata
thawabu. Lakini hata hivyo, juzi serikali ya Iran ilikuwa ikifanya
utaratibu wa kurudisha miili ya marehemu wake nchini Iran kwa mazishi.
Mungu aziweke pema peponi, roho za marehemu wote. Amina.
Imeandikwa na Makongoro Going,’ Haruni Sanchawa na Issa Mnally.
Imeandikwa na Makongoro Going,’ Haruni Sanchawa na Issa Mnally.
Note: Only a member of this blog may post a comment.