Saturday, September 12, 2015

Anonymous

AL-SHABAAB Waua Polisi, Raia Kibao!

AlShabaabfighters014.jpg
ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Wiki iliyopita nilieleza jinsi ambavyo Mtanzania, Vedasto Nsanzukwanko alivyojeruhiwa vibaya kwenye Shambulio la Al-Shabaab katika Maduka ya Westgate Mall jijini Nairobi, Kenya. Pia tuliona jinsi mpwa wa Rais Uhuru Kenyatta, Mbugua na mchumba’ke, Rosemary walivyopoteza maisha walipokwenda kwenye maduka hayo kununua pete kwa ajili ya maandalizi ya ndoa yao.
SASA ENDELEA…
Wakati Kenya wakitafakari tukio hilo, taarifa mpya zilienea kwamba, polisi wawili nchini humo walikuwa wameuawa na watatu kujeruhiwa vibaya baada ya kuvamiwa na Al-Shabaab.

Zilikuwa ni habari mbaya mno kwani tukio hilo lilijiri wakati Wakenya wakiwa katika maombolezo ya siku tatu kuwakumbuka watu zaidi ya 60 waliopoteza maisha na 175 kujeruhiwa katika shambulio la kwenye jengo la biashara la Westgate.

Shambulio hilo lilitokea katika kituo cha ulinzi kilichopo karibu na mpaka wa Somalia mjini Mandera na kuibua hofu nyingine mpya.

Kamanda wa Polisi, Charlton Mureithi alinukuliwa kuwa, mbali na polisi wawili kuuawa na watatu kujeruhiwa, pia kundi hilo lilikuwa limechoma magari 11.

Ilikuwa ni saa chache tu baada ya Kundi la Al-Shabaab kutoa taarifa kuwa mashambulio mengine yataendelea hadi Kenya watakapoondoa wanajeshi wake nchini Somalia.

Aliyetajwa kuwa kiongozi wa kundi hilo korofi, Ahmed Godane alitoa onyo kwa Wakenya kuwa hakuna njia yoyote wangeweza kuhimili vita ya kulipa kisasi ndani ya nchi yao wenyewe. Katika taarifa yake iliyochapishwa mitandaoni kabla ya vyombo vya habari, kiongozi huyo alinukuliwa: “Chagua kuondoa majeshi yenu yote… Vinginevyo jiandae kwa wingi wa damu itakayomwagika nchini kwenu, anguko la kiuchumi na makazi.”

Wakati hilo likijiri, ghafla kuliibuka habari nyingine mbaya zaidi kuwa Al-Shabaab walikuwa wameua abiria 28 Kaskazini-Mashariki mwa Kenya.

Polisi walisema watu waliokuwa na bunduki, wanachama wa Kundi la Al-Shabaab walivamia basi moja na kuua abiria 28 ambao hawakuwa Waislam ambao walichaguliwa kati ya abiria 60 waliokuwa ndani ya basi hilo.

Kundi la wanamgambo wa Kisomali la Al-Shabaab lilidai kuhusika na shambulizi hilo likisema ni majibu kwa uvamizi wa majeshi ya usalama ya Kenya uliofanywa katika misikiti mjini Mombasa.

Maafisa hao walisema wanamgambo walilikamata basi hilo kiasi cha kilometa 50 kutoka Mji wa Mandera karibu na mpaka wa Kenya na Somalia.

Kuanzia hapo, Kenya iliendelea kukumbwa na mlolongo wa mashambulizi ya silaha na mabomu ambayo yalidaiwa kufanywa na wanamgambo wa Al-Shabaab wenye uhusiano na Al-Qaida tangu Kenya ipeleke majeshi yake nchini Somalia mwaka 2011.

Wanajeshi wa Kenya ni sehemu ya tume ya ulinzi wa amani ya Umoja wa Afrika nchini Somalia ambayo inaisaidia serikali dhaifu ya Somalia ambayo inaungwa mkono na Umoja wa Mataifa ili kupambana na uasi wa Al-Shabaab nchini humo.

Wakati upepo haujatulia, ghafla kuliibuka habari nyingine kuwa takriban watu 36 walikuwa wakihofiwa kufariki dunia katika shambulio lililotokea kwenye machimbo ya kokoto karibu na Mji wa Mandera, Kaskazini mwa Kenya.

Wakazi wa eneo hilo waliripoti kuwa waathirika wote wa tukio hilo walikuwa ni watu wasio Waislam ambao walikuwa wakifanya kazi katika machimbo hayo yaliyopo Kormey, kilomita 15 kutoka Mji wa Mandera.
Kundi la wapiganaji wa Kiislam la Al-Shabaab lilikiri kuhusika na mauaji hayo ya kila kukicha.
Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia wiki ijayo.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.