Friday, August 28, 2015

Anonymous

TAHADHARI: Baada ya DAR na MOROGORO Sasa KIPINDUPINDU Chapiga Hodi Mkoa Huu....

Baada ya kushambulia mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro, ugonjwa wa kipindupindu sasa umepiga hodi katika Mkoa wa Pwani na tayari watu tisa wameonekana kuwa na dalili za ugonjwa huo. 

Hali hiyo imeulazimu uongozi wa idara ya afya mkoani Pwani kutenga maeneo ya kuwalaza kwa ajili ya vipimo na tiba huku katika Mkoa wa Dar es Salaam ugonjwa huo umewakumba watu 348 na vifo 10. Juzi, Mkoa wa Morogoro uliripotiwa kuwa na wagonjwa 32 huku mmoja akiwa tayari amepoteza maisha. 

Wakati wagonjwa katika mikoa hiyo wakizidi kuongezeka, Ofisa Afya wa Mkoa wa Pwani, Simon Malulu alisema mtu mmoja amethibitika kuugua kipindupindu huku wengine wanane wakilazwa kwa kuwa na dalili za ugonjwa huo. 

Alisema Agosti 18, kulikuwa na wagonjwa wawili kutoka Bagamoyo na wamekuwa wakiongezeka kutoka Mkuranga, Kibaha Vijijini na Kibaha Mjini.
Alisema mara ya mwisho, ugonjwa huo uliikumba Pwani mwaka 2005. 

Wakati huohuo; Manispaa ya Kinondoni imetumia polisi kuwakamata baba na mama lishe wanaokiuka agizo la kutokufanya biashara ya chakula kipindi hiki cha mlipuko wa kipindupindu.
Ofisa afya manispaa hiyo, Mathias Kapizo alisema wamelazimika kuchukua hatua hiyo baada ya kuona idadi ya watu wagonjwa inaongezeka. Alisema wamepokea wagonjwa wapya 35 na kufanya idadi yao kufikia 52.
Waandishi wetu waliotembelea Soko la Mapinduzi, Mwananyamala waliwakuta mama lishe wakiendelea na biashara hiyo. 

Mwenyekiti wa soko hilo, Hamis Marande alisema maofisa wa afya hawajawapa taarifa yoyote na hawajasikia tangazo linalokataza kuuza chakula badala yake maofisa wanapita kudai Sh5,000 kwa ajili ya kupima afya.
Katika hatua nyingine, Manispaa ya Ilala imewatoza faini ya Sh50,000 wafanyabiashara waliokaidi agizo la kuuza chakula katika mazingira machafu. 

Mganga mkuu wa manispaa hiyo, Victorina Ludovick alisema: “Hatutatumia nguvu kubwa lakini eneo hili lina watu wakorofi ndiyo maana tumeongozana na mgambo.” Alisema juzi, walipokea wagonjwa wapya wanne na walioko kambini ni 14 na kufanya idadi ya watu waliougua ugonjwa huo kufikia 60 katika manispaa hiyo.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.