Mke wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Regina, amesema anashindwa kuelewa ni kwanini watu wanatunga uongo kuhusu mumewe.
“Huyu ni mume wangu, namfahamu kulikoni mtu mwingine yeyote… ni mchapakazi, ni mtu anayethamini utu, mpenda maendeleo, asiyependa unyanyasaji. Nashindwa kuelewa kwanini watu wamtungie uongo badala ya kuja kwangu kuniuliza,”.
Akizungumza huku akishangiliwa na wanawake waliohudhuria mkutano huo na kulazimu mshereheshaji muda wote kuingilia kati kuwaomba kunyamaza, Regina alisema kila mmoja afanye mabadiliko pamoja na kufika viwanja vya Jangwani kesho ambapo uzinduzi wa kampeni za Ukawa utafanyika.
Regina alisema kuwa amefarijika kuzungumza na wanawake na mabinti wa Tanzania kwa kuwa wao ndio chimbuko la maendeleo.
“Taifa linapaswa kufanya mabadiliko ya kweli ili kufikia maendeleo, na yatafanywa na wanawake… Kuna sheria nyingi ambazo zinamnyima mwanamke nguvu kama vile sheria ya kumiliki mali, wakati umefika wa kufanya mabadiliko. Ni wakati wa mabinti kuacha kudhalilishwa, wakati umefika kina mama kumiliki mali, huduma bora za jamii, afya, elimu nk,”.
Alisema wanawake ambao wanazalisha zaidi kuliko wanaume hawana manufaa na mazao wanayoyapata kutokana na kushindwa kuwezeshwa.
“Nadhani kuna umuhimu wa kubadilisha sera za kilimo, ufugaji na hilo litasaidia mabadiliko, sensa inaonyesha wanawake ni wengi na hivyo ni jeshi kubwa tukiamua kuleta mabadiliko tunaweza,” alisema.
Akihutubia umati huo wa wanawake, Lowassa alisema anadeka kutokana na mafuriko ya wanawake ndani na nje ya ukumbi huo ambayo yalisababisha rafiki yake kutoka Zanzibar kumweleza kuwa si mapenzi bali ni mahaba.
“Nadeka, hizi ni baraka za mwenyezi Mungu na sio mkono wa mtu, rafiki yangu wa Zanzibar aliwahi kuniambia haya si mapenzi bali ni mahaba. Sasa nawapeni kazi, nimekuwa mbunge kwa miaka 30, wanawake ni waaminifu, wakisema wanakupa kura wanakupa, naomba mnitafutie kura, nataka kura za kutosha kuwashangaza Watanzania, sio kura yako tu bali pia ya mume, watoto na mtu mwingine,” alisema.
Lowassa ambaye muda wote alikuwa akishangiliwa, alisema kuna ambao wanaona kuwa ameingia kwenye mchezo kwa kucheza, na kwamba watashangazwa na sanduku la kura Oktoba 25.
“Kila mwanamke anayenisikiliza naomba anipatie kura na tukimaliza kazi ya kura tutakutana Arusha Ngurdoto Desemba kama tulivyo. Halima na Mbowe tumezungumza jambo hilo, tukae mahali tujadili mabadiliko maana yake nini, nataka kupeleka maendeleo kwa kasi ya ajabu,” Lowassa.
Alisema mabadiliko nchini hayaepukiki, kwani mwaka 1995 Nyerere aliuambia mkutano wa Chama Cha Mapinduzi kuwa Watanzania wanataka mabadiliko na wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje.


Note: Only a member of this blog may post a comment.