Watu tisa wa familia moja wameteketea kwa moto baada ya nyumba yao
kuungua usiku wa kuamkia jana jijini Dar es Salaam, huku mashuhuda
wakisema walikuta miili yao ikiwa imeshikana.
Walioteketea katika tukio hilo ni mama wa familia hiyo, Samira Juma Ibrahim (42), maarufu kwa jina la Mama Aisha na watoto wake wanne, Ahmed Masoud (15) aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza, Aisha Masoud (17), aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la sita, Abdillah Masoud (10) na Ashraf Masoud (5).
Wengine ni Bimdogo Masoud (72), ambaye alikuwa mgonjwa na mama wa Samira, pamoja na wadogo zake wawili wa kike, Samira Harood (17) na Wahat Saleh (27), ambaye alitokea Unguja, pamoja na Fahir Fesal mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema baada ya kusikia kelele za vilio, waliizunguka nyumba hiyo kwa lengo la kutaka kuwaokoa, lakini ilishindikana baada ya milango kutofunguka na moto kuwa mkali kiasi cha kushindwa kuingia.
“Katika namna ya kujaribu kujiokoa, Ahmed alijaribu hata kurusha nje funguo ili waweze kufunguliwa mlango, lakini ilishindikana. Hivyo alirudi chumbani wakashikana pamoja kusubiri kifo,” Suleiman Bashraf ambaye ni kaka wa Samira.
Bashraf, anayeishi Mikocheni na ambaye anasema alifika eneo la tukio wakati dada yake na watoto wake wakiwa wameshafariki, alibainisha kuwa baba wa familia hiyo, Masoud Materu ambaye ni mfanyakazi wa kampuni ya Kimataifa ya Huduma za Kontena (TICTS) inayofanya kazi kwenye Bandari ya Dar es Salaam, alikuwa kazini wakati wa tukio hilo.
Alisema alipopigiwa simu hakuelezwa kuhusu tukio hilo, badala yake wafanyakazi wenzake walimsindikiza hadi Msikiti wa Ulam na baadaye saa tatu asubuhi alipelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako maiti za waliofariki zimehifadhiwa.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema wamepokea taarifa ya tukio hilo na jeshi hilo linaendelea na uchunguzi.
Shuhuda mmoja wa tukio hilo, Hassan Banda alisema ingawa alifika eneo hilo mapema, walishindwa kuingia ndani kuwa mlango wa nondo haukuweza kufunguka.
Alisema baadaye, mmoja wao aliruka ukuta lakini alikuta hali ni mbaya kwani mlango wa nyuma wa kutokea jikoni ndiko moto ulikuwa umeanzia na ulikuwa mkali sana, hivyo akalazimika kurudi upande wa mbele.
“Kuna kijana mmoja (marehemu Ahmed) ndiye tulikuwa tukiwasiliana naye tukimpa maelekezo akiwa ndani ya nyumba. Tulimwambia alete chuma cha kuvunjia, lakini akaleta funguo na kuurusha nje. Kwa kuwa kitasa kilishapata moto ilishindikana kufungua,” alisema.
“Baadaye akasema anakwenda chumbani kwa bibi yao. Waliendelea kulia wakihitaji msaada, lakini baadaye kukawa kimya na hapakuwa na mawasiliano tena.”
Shuhuda huyo alisema muda mfupi baadaye walisikia kishindo kikubwa cha kulipuka kwa mtungi wa gesi na kisha paa la nyumba likashuka chini, lakini akasema wakati huo tayari watu wote walishafariki dunia.
Marehemu walizikwa jana kwenye Makaburi ya Kisutu baada ya ibada iliyofanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
-MWANANCHI


Note: Only a member of this blog may post a comment.