Stori: Dustan Shekidele
Ni maajabu ya Mungu! Nyuma ya tukio la ajali ya basi kugona treni iliyotokea hivi karibuni, yamebainika maajabu ya aina yake baada ya mtoto Alhaji Mdoe aliyekuwa amepakatwa na mama yake kukutwa akiwa hai wakati mama yake akiwa amefariki dunia.Akizungumzia tukio hilo, baba wa mtoto huyo, Mdoe Ally, mkazi wa Kijiji cha Tingiga, Kilosa, alisema kwenye basi hilo alikuwa yeye na familia yake akimpeleka mkewe Amina Mohamed kwa mganga Mlandizi Mkoa wa Pwani aliyekuwa akisumbuliwa na maradhi ya miguu na mikono.
“Nilikuwa safarini kwenda Mlandizi kumpeleka mke wangu kwa mganga kwa bahati mbaya wote tumejeruhiwa isipokuwa mtoto wangu mdogo Alhaji ambaye alibebwa na mama yake (mkewe), Husna na Salehe (wanaye) wamevunjika miguu na mama yao ameumia kichwani,” alisema Mdoe ambaye kwa wakati huo (juzi), alifichwa kama mkewe alifariki kwenye ajali hiyo.
Mganga Mfawidhi wa Hospital ya Wilaya Kilosa, Dk. Dikson Masale amethibitisha kupokea maiti 5 na majeruhi 31.
“Ni kweli tumepokea majeruhi 31 kati yao wanaume 10, wanawake 15 na watoto 6 na maiti 5 ambazo zimetambuliwa kwa majina ya Saleh Gomba, Amina Mohamed, Mwajili Mzange, Surati Mwajili na dereva wa basi hilo, Masoud Cholo,” alisema Dk. Masale.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Mussa Malambo amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo iliyohusisha gari lenye namba za usajili TB37 CMT Isuzu Coaster lililogonga treni.

Note: Only a member of this blog may post a comment.