Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe, amenusurika kifo baada ya ndege aliyokuwa
akisafiria kutoka Iringa kwenda Zanzibar kutaka kugongana uso kwa uso na
ndege nyingine dakika moja kabla ya kutua.
Waziri Membe akiwa na ujumbe wake wa watu wanane, walikuwa wakisafiria ndege ya kukodi kampuni ya 5H NEG Precition Aviation ikirushwa na rubani Mathew Mhahiki, ambaye ameonyesha kushangazwa na tukio hilo alilodai “ni kwa rehema za Mungu tumepona ajali hii.”
Waziri Membe alisema: “Nina uzoefu mkubwa
wa kusafiri na ndege mahali pengi duniani, hali hii ilikuwa ni ajali na
labda sasa tungekuwa dead bodies, lakini ninajua Mungu yuko upande wetu
katika safari hii ya uhakika, lakini pia izingatiwe nimekuja kufanya
kazi ya Mungu.”
“Katika safari hii tutashuhudia mambo
mengi sana, lakini kwa kuwa kila ninapotaka kuondoka nyumbani ama
hotelini mara nyingi nimekuwa nikimtanguliza Mungu maana bila Mungu hii
ilikuwa ni mwisho wa maisha yetu tuliokuwa kwenye ndege hii.”
Waziri Membe alikuwa amealikwa mjini hapa na Umoja wa Akimama wa Kikristu (Umaki) wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Zanzibar waliokuwa wakifanya mkutano wao mkuu unaofanyika kila baada ya miaka mitano akitokea Iringa ambako alikwenda kutafuta udhamini wa chama ili kumwezesha kugombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi, CCM.
Akiwa uwanjani hapo, Waziri Membe
alikutana na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba aliyekuja hapa
Zanzibar kutafuta wadhamini ambapo makada hao walipata nafasi ya
kuzungumza.
Akiwa katika mkutano huo, Waziri Membe
alisema: "Miongoni mwa mambo yanayonikera ndani nafsi yangu ni kuona
mwanamke bado anaachwa nyuma, hili halipendezi, ni lazima tuhakikishe
wanawake wanapata elimu ya ufundi stadi maana mwanamke akiwezeshwa hasa
katika eneo hili la elimu wanaweza hata kushinda wanaume wengi.”
“Ni lazima kina mama wawezeshwe kujiajiri
ili msiwategemee kina baba kwa kila jambo lakini pia ili kufikia
malengo hayo ni lazima tuwape elimu kina mama.”
NA KAJUNA BLOG


Note: Only a member of this blog may post a comment.