Tuesday, June 16, 2015

Anonymous

MDADA SHTUKA! ZINGATIA HAYA KWA MUMEO TAFADHALI!

Shoga zangu, ni matumaini yangu kwamba nyote mtakuwa na afya njema na mapambano ya maisha yanaendelea vizuri licha ya kuwa na changamoto za hapa na pale.Kwa upande wangu ondoeni shaka, afya yangu ni njema na mume na watoto wetu wapo poa kabisa.

Leo shoga zangu nimeamua kuzungumza nanyi kuhusu uzembe unaofanywa na baadhi ya wenzetu baada ya kupata watoto na kusahau kabisa majukumu yao kwa waume zao.Nimeamua kuzungumza nanyi ishu hii kwa sababu ina madhara makubwa katika ndoa na baya kuliko yote ni pale ‘mkuu wa kaya’ anapoamua kukutelekeza wewe na mtoto na kwenda kupiga kambi kwa nyumba ndogo.

Tukio hilo linaweza kutokea miaka michache tu tangu mlipofunga ndoa na kuwaacha watu wakiwa wamepigwa na butwaa kwa kutoamini ndoa yenu ya kifahari ilivyoshindwa kudumu, kisa mama kuwa bize na mtoto kuliko aliyesababisha mtoto huyo kupatikana.

Shoga zangu, mada hii siyo ngeni sana kujadiliwa lakini kwa kuwa safu hii ni mahususi kwa ajili ya kuhakikisha ndoa hazivunjiki nimeamua kuwakumbusha kwani kukumbushana ni jambo zuri.Ni hivi shoga zangu, utamkuta mwanamke kabla ya kujaliwa kupata mtoto anakuwa bize sana mumewe kumjulia hali kwa kumpigia simu au kumtumia ujumbe mtamu mara kwa mara.

Haishii hapo, atataka kujua kila kitu ambacho mumewe anakifanya na kumuahidi kumpa mapenzi shatashata akirejea nyumbani au kumweleza awahi kurudi kwa sababu kampikia chakula kizuri nk.Wakati akimsubiri mumewe, mwanamke husika kama kawaida yake atakuwa kapendeza huku kafanya usafi wa nyumba kwa asilimia mia moja mambo ambayo mumewe anayapenda.

Tatizo linakuja pale mwanamke huyo anapojaliwa kupata mtoto, muda wote atakuwa bize na mwanaye hamjulii hali mumewe akiwa kazini, akirejea nyumbani hampokei na usiku wanalala mzungu wa nne yeye yupo bize tu na mwanaye.
Shoga, ngoja nikuulize, hivi huyo mtoto aliyesababisha aje duniani ni nani kama siyo mumeo? Kama ndiye kwa nini usigawe muda wa kuwa bize na mtoto ili naye apate nafasi ya kufurahi na wewe?

Kitendo cha wanawake kutokuwa karibu na waume zao wanapopata watoto, kutojiweka safi kwa madai ya kulea huwafanya wanaume kutowapenda wake zao na kuamua kutafuta ‘vidosho’ ambao watakuwa wakifurahia nao maisha wakati wao wakilea.

Cha msingi shoga zangu, mnapokuwa na watoto mshukuruni Mungu kwa kuwapatia zawadi hiyo ya pekee na wawe chachu ya ninyi kuongeza mapenzi kwa waume zenu kinyume cha hapo mtatelekezwa na watoto wenu. Bye.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.