Sunday, January 1, 2017

Unknown

Mwaka Mpya 2017: Mashine za EFDs ‘Kumwagwa’ Nchini!

ILI kuongeza mapato, serikali inatarajia kusambaza kwa wingi mashine za kielektroniki za Mamlaka ya Mapato (EFDs) mwaka huu.
Lengo la hatua hiyo ni kusimamia dhana ya kulipa kodi kwa hiari na kuendelea kuboresha makusanyo ya kodi mbalimbali, zinazotozwa na serikali. Lengo pia ni kuboresha makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi, hasa yale yanayotokana na michango ya mashirika na wakala za serikali.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango alisema hayo alipokuwa akitoa Mwelekeo wa Matarajio hadi Juni 2017.

Mbali na hayo, alisema Serikali itaendelea na majadiliano baina ya Serikali na wahisani ili kuhakikisha kwamba fedha za misaada na mikopo, zinapatikana kama ilivyopangwa.

Vile vile itaendelea kufanya uthamini wa mkupuo wa majengo ili kukusanya zaidi kodi ya majengo. Pia, itatoa elimu juu ya umuhimu na faida za kulipa kodi kwa kutumia mitandao ya kielekrtroniki.

Dk. Mpango alisema Serikali pia inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuendelea kusisitiza nidhamu katika utekelezaji wa bajeti, kama ilivyoidhinishwa kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015.

“Pia tutaendelea kuwianisha mapato na matumizi kwa kuhakikisha kuwa mgawo wa fedha unaendana na upatikanaji wa mapato, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima kama kupunguza safari za nje zisizo na tija na matumizi katika sherehe za kitaifa na makongamano,” alisema Dk. Mpango.

Aidha, aliwajulisha wafanyabiashara kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inathamini mchango wao katika maendeleo ya nchi, hivyo milango ya Serikali ipo wazi kwa wale wote wenye hoja zenye maslahi kwa Taifa.

Alisema wizara yake imeshatoa tangazo kwa watanzania na wadau wote wa kodi, kuwasilisha mapendekezo ya marekebisho ya kodi kwa ajili ya uchambuzi na kufikiriwa kuingizwa katika mapandekezo ya mabadiliko ya kodi katika bajeti ijayo.

Aliwaomba wadau wote, kuitumia vizuri fursa hiyo ili yapatikane mapendekezo mazuri ya kuboresha mfumo wa kodi, utakaoipatia Serikali mapato zaidi ya kuendeleza nchi. Kuhusu deni la Taifa, alisema deni la ndani liliongezeka kufikia Sh. bilioni 10,089.3 mwishoni mwa Oktoba mwaka jana kutoka Sh. bilioni 8,597.0 Desemba mwaka juzi.

“Ongezeko hilo lilitokana na serikali kukopa kupitia dhamana na hati fungani kwa ajili ya kugharamia bajeti ya serikali kwa mwaka 2015/16 ikichangiwa pia na kupungua kwa misaada na mikopo kutoka nje,” alisema.

Waziri Mpango alisema pamoja na kuongezeka huko, deni la taifa bado ni himilivu. Uchambuzi wa uhimilivu wa deni uliofanyika mwezi Novemba mwaka huu unaonesha kuwa viashiria vya deni la nje na deni lote la umma, vitaendelea kuwa chini ya ukomo wa uhimilivu kwa kipindi cha muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu.

Alieleza kuwa pamoja na mafanikio, zipo changamoto kwa baadhi ya wafanyabiashara na wananchi, ambazo ni kutokuwepo kwa mwamko wa matumizi ya mashine za kielektroniki, ukusanyaji usioridhisha wa maduhuli ya serikali, kushindwa au kuchelewa kupatikana kwa mikopo yenye masharti nafuu na ya kibiashara kutoka nje, maombi ya misamahaa ya kodi na mahitaji makubwa yasiyowiana na hali halisi ya upatikanaji wa mapato.

Katika hatua nyingine, alisisitiza kuwa uamuzi wa serikali kuzitaka taasisi za umma kufungua akaunti ya mapato Benki Kuu (BoT), utaendelea kubaki kama ulivyo.

“Fedha hizi za umma zilikuwa zikitumika vibaya na bodi za mashirika, lakini pia zilitumika kuikopesha serikali fedha zake yenyewe kwa riba kubwa kupita biashara ya dhamana na hati fungani za serikali. Kasoro hiyo iliondoa motisha kwa mabenki ya biashara kupeleka huduma za kifedha vijijini na hata kukopesha sekta binafsi,” alisema.

Alisema ni vema watanzania wafahamu kuwa akaunti ambazo fedha za mashirika, zimehamishiwa Benki Kuu ni akaunti za kukusanya mapato tu. Alisisitiza kuwa akaunti za matumizi, bado ziko katika benki za biashara ili kuwezesha mashirika kufanya malipo kupitia akaunti hizo.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.