Haruni Sadiki aliyecharangwa mapanga na mdogo wake.
Gabriel Ng’osha
Inasikitisha sana! Kijana Haruni Sadiki (24), mkazi wa Jangwani,
Dar, amenusurika kuuawa kwa kucharangwa mapanga na mdogo wake aitwaye
Abdurazaki Bakari ‘Riziki’ (22).
Akizungumza akiwa na maumivu makali kwenye Hospitali ya Muhimbili,
Haruni aliliambia gazeti hili kuwa chanzo cha tukio hilo ni ugomvi
uliotokea kati ya wanandugu hao.
Sehemu ya jeraha kichwani mwa Haruni Sadiki aliyecharangwa mapanga.
“Kuna mdogo wetu anaitwa Hemed (5), alikuwa na tabia ya kukojoa
kitandani. Nakumbuka siku ya tukio yule mtoto alikojoa kama kawaida
ndipo ukaibuka ubishi kati ya Riziki na kaka yetu mwingine aitwaye
Nasri.
“Nasri alitaka Hemed (aliyekojoa) atembezwe mtaani na godoro kichwani
huku akipigiwa ngoma lakini Riziki hakutaka mtoto afanyiwe hivyo badala
yake alitaka ampige ndipo ukaibuka utata kati yao.
Mtuhumiwa, Abdurazaki Bakari ‘Riziki’
“Baada ya malumbano, walijikuta wakigombana ndipo nikawaamulia.
Katika kuwaamulia nikampiga ngumi Riziki kwa bahati mbaya, jambo
lililomchukiza na kuahidi kulipiza kisasi.
“Maisha yaliendelea kama kawaida Riziki akiwa na kinyogo hadi
aliponiomba twende sehemu tulivu tuzungumze jambo, nikakubali, cha ajabu
akawa ananipeleka kwenye jumba bovu.
“Tulipofika kwenye jumba hilo alianza kunipiga na kuniuliza kwa nini
nilimpiga ngumi, nilijua ni utani, nikamsukuma akaanguka ndipo akachomoa
panga kiunoni na kunicharanga.
“Alinikata kisogoni, nikaanguka, akanikata vidole viwili vya mguuni, alipoona napiga mayowe ya kuomba msaada akatoweka.
“Bahati nzuri wasamaria wema walinikimbiza Hospitali ya Amana kisha
nikahamishiwa Muhimbili ambapo iliwalazimu kumalizia nusu ya kiganja
kilichokuwa kinaning’inia,” alisema Haruni.
Mtuhumiwa amefunguliwa jalada la kesi Namba ILA/RB/3847/15- SHAMBULIO LA KUDHURU MWILI na anasakwa na polisi.

Note: Only a member of this blog may post a comment.