Lakini baada ya kufikiri kidogo,
nimegundua wengi wa wenzangu, maana yao ya mabadiliko ni kukiondoa chama
tawala madarakani, bila kujali mema au mabaya yatakayotokea katika
maisha yao binafsi baada ya jambo hilo kutokea.
Huu unaweza kuwa mjadala unaoweza kujadiliwa wakati mwingine, kwani kwa leo nadhani kitu cha muhimu zaidi kukijadili kama taifa, ni kauli iliyotolewa na mgombea urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Ngoyai Lowassa aliyoitoa mwishoni mwa wiki iliyopita, akiwa kanisani mjini Tabora.
Lowassa, Mkristo wa dhehebu la Kilutheri, aliwaambia mamia ya waumini waliokuwa kanisani kuwa baada ya Wakatoliki wawili kuiongoza Tanzania kwa vipindi tofauti (Julius Nyerere 1961-1985 na Benjamin Mkapa 1995-2005) sasa ni zamu ya Mlutheri kupata ridhaa ya Watanzania kuwaongoza kutokea ofisi yetu namba moja iliyopo Magogoni, jijini Dar es Salaam.
Wapo baadhi yetu wanaweza kuliona jambo hili kama ni dogo, lisilopaswa kupewa uzito. Watanzania wengi wana tatizo la kupuuza masuala ya msingi na kushupalia mambo madogo. Wanapenda zaidi kujadili watu binafsi badala ya hoja.
Kwamba Walutheri sasa waombe ili mtu wao aende ikulu siyo suala dogo, kwa sababu kauli hiyo imetolewa na mtu anayetaka kuwa rais wa nchi. Ni wazi kuwa, katika kipindi chote cha maisha yake, ameshuhudia asichokipenda kikiendelea dhidi ya watu wa dhehebu lake na labda ameona mengi ya upendeleo wakitendewa watu wa Kanisa Katoliki!
Unapokutana na mtu mwenye mawazo kama haya, ni vigumu kujizuia kufikiri kuwa huenda, kwa miaka yote hajawahi kuona rais wa nchi akitokea kabila lao, mkoa wao au hata ukanda wao!
Katika ulimwengu wa kutanguliza nafsi yako kwanza, siyo vibaya wala dhambi mtu kuwaza namna hii, kwa vile ni binadamu wachache walio tayari kuwapa wenzao kabla yao. Hata hivyo, hulka hii hukutana na vikwazo kwa kadiri mtu anavyokomaa kiakili, kiuchumi na kijamii.
Kijamii, unapokuwa mtu unayetazamwa na watu wanaokuzunguka, iwe kutokana na uwezo wako kifedha, kiuongozi au hata kwa umri, kuna mambo unazuiwa kuyatamka au kuyatenda hadharani.
Lowassa anatafuta urais wa Watanzania wote, anapotoa kauli kama hii, tena katika kanisa lao, anajenga aina f’lani ya ubaguzi wa kiimani. Kama tumepata kuwa na viongozi Wakristo Wakatoliki wawili, kumbe baadhi ya madhehebu hayajawahi kupata hata waziri mkuu!
Kwa maana hiyo, Walutheri, Waprotestanti, Waanglikana nao wanahitaji kuwa na kiongozi kutoka kwao. Kama ni hivi, basi hata Waislamu wa Sunni, Shia au Wahamadiya nao watahitaji ‘mukulu’ anayetokana na wao.
Kama tutajibagua kwa misingi hii, upo uhakika kwamba baadhi ya madhehebu hayataweza kutoa rais wa Tanzania milele kutokana na udogo wao. Vivyo hivyo kwa wale wanaolenga ukabila, ukanda au elimu.
Kama tutafikia wakati wa kuomba kuungwa mkono na Watanzania wa jamii f’lani, kwa sababu tu mtu ana unasaba nayo, hili ni kosa lisilofaa kufumbiwa macho wala kuona aibu kulikemea. Watanzania ni watu waliojichanganya mno kiasi kwamba ukabila, udini, chama cha siasa, utajiri wala elimu haujawahi kuwa msingi wa mtu kupendwa au kuchukiwa.
Mtu anachukiwa au kupendwa kwa matendo yake. Tusianze kusingizia dini zetu, madhehebu yetu, makabila yetu au ukanda tunaotoka katika kuhalalisha jambo lolote. Ni wajibu wa viongozi kuonesha mshikamano wa Watanzania kwani udini ni sumu katika taifa letu, tukiuendekeza utaleta mfarakano.

Note: Only a member of this blog may post a comment.