Monday, September 7, 2015

Anonymous

TABIA; SILAHA MUHIMU INAYOWEZA KUJENGA, KUBOMOA UHUSIANO


JUMAMOSI nyingine wapenzi wasomaji wa safu hii tunakutana katika uwanja wetu wa kuweza kupata elimu ya uhusiano. Mapenzi yanachukua nafasi kubwa katika maisha yetu ya kila siku. Bila mapenzi, watu wasingezaana na hata furaha ya maisha isingekamilika kama hakuna mapenzi.

Niwashukuru wale wote ambao mlinitumia ujumbe mfupi, mkipongeza kwa mada ya wiki iliyopita iliyokuwa ikifundisha mbinu mbalimbali za kumpata mchumba mwema. Mliipenda na hata wengine mkitaka niirudie, nitafanya hivyo siku nyingine Mungu akipenda.

Leo tuitazame mada iliyopo hapo juu. Hakuna asiyetaka kuwa na penzi tamu. Mtu unapofurahia penzi tamu kutoka kwa mpenzi wako, kila kitu kinakwenda vizuri. Ili wapendanao waweze kudumu na kufurahia uhusiano, wanapaswa kwanza kusomana tabia.

Vijana wengi kwa sasa wanapoingia kwenye uhusiano, suala la tabia huwa hawalizingatii. Mtu anachoangalia ni furaha ya matamanio. Kama ni mwanaume anatafuta mwanamke mzuri kwa kuangalia uzuri wa sura na umbo.
Anataka mwanamke ambaye akisimama mbele ya marafiki zake, wamuambie ‘hongera bwana naona una kifaa kwelikweli.’ Anataka mwanamke wa maonesho. Akitoka naye viwanja vya starehe ajione yeye ndiyo yeye. Si sahihi, tunajiongopea.

Vivyo hivyo kwa mwanamke. Naye anaangalia mwanaume ambaye ana uzuri wa sura. Mtanashati ambaye akitembea naye barabani kila mtu amuone yeye amepatia. Anajua kuchagua, ana mwanaume mzuri. Kwamba ana mwanaume ambaye anaweza kumtambulisha kwa marafiki zake. Anaweza kutoka naye ‘out’ sehemu mbalimbali.

Bila kujua anakosea. Anafikiri kwamba yupo sahihi. Ainjoi safari ya mapenzi akiwa gizani. Anafikiri ataishi na mtu huyo hadi kufikia hatua ya kufunga ndoa. Kabla hajafika mbali, kutokana na sababu anazozijua, mwenzake anahamia kwingine. Anaachwa solemba.

Ndugu zangu, kabla ya kuanzisha uhusiano na mtu yeyote, anza kushughulikia suala la tabia kwanza kisha mambo mengine ndiyo yafuate.Uzuri uwe ni sifa ya pili. Sifa ya kwanza kabisa ya kutaka kuanzisha uhusiano na mtu ni kumchunguza tabia. Unaweza kumjua mtu tabia yake kabla na hata baada ya kuanzisha uhusiano. Mchunguze kwa makini mtu unayetaka kuanzisha naye uhusiano, ana tabia njema? Ana hekima, ana busara? Ana hofu ya Mungu? Ana ustamilivu wa kuishi katika shida na raha? Anajua utu?

Usikubali kuanzisha au kuendeleza safari na mtu ambaye hana tabia njema. Japo tabia ya mtu waweza kumbadilisha lakini ni vyema ukaliangalia mapema suala la tabia maana Waswahili wanasema nyota njema inaonekana asubuhi.
Huwezi kupata tabia njema kwa mtu ambaye amelelewa kwenye maadili mabaya. Huwezi kupata tabia nzuri kwa mtu mhuni. Mtu wa kukaa kwenye vijiwe vya kuvuta bangi, hawezi kuwa na tabia njema hata siku moja. Mtu ambaye ni wa kukesha kwenye starehe kila uchao, sherehe ilipo ndipo na yeye yupo, atafaa huyo kuwa mchumba wako?

Unaweza pia kumsoma mtu tabia hata ikiwa tayari mmeshaanzisha uhusiano. Unapaswa pia kuhakikisha je, tabia alizonazo mnaweza kuendana? Mnaweza kwenda sawa. Tabia zake na zako zinafanana au ni kama ardhi na mbingu?
Fanya tathmini ya kina kabla ya kuamua kuendelea na safari. Maamuzi yako yanapaswa kufanyika wakati umeshajiridhisha vya kutosha kwamba mwenzako mnaendana tabia na kama kuna baadhi ya vitu mnapishana basi viwe vidogovidogo ambavyo mnaweza kuvirekebisha na safari yenu ikaendelea vizuri.

Ukiona tabia hamuendani. Mwenzako amezidiwa na tamaa za mjini, hawezi kubadilika ni vyema ukaachana naye na kusubiri umpate yule ambaye atakuwa ni sahihi kwako. Marafiki, mtu unayepanga kuwa mchumba na baadaye mke lazima ujiridhishe mara mbili kabla ya kuamua.

Mtu ambaye utaishi naye maisha yako yote, lazima awe mtu mwenye tabia njema. Awe na hofu ya Mungu. Atakayejua shida na raha. Asiwe mtu wa raha tu linapotokea tatizo anakimbia. Awe kweli jasiri atakayekuwa tayari kwenye ugumu na utamu wa maisha.

Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri!

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.