Monday, September 7, 2015

Anonymous

AL-SHABAAB WAJERUHI MTANZANIA, WAMUUA MPWA WA RAIS KENYATTA!

Wiki iliyopita tuliona ripoti ya vifo vya kutisha katika Maduka ya Westgate Mall kwenye Jiji la Nairobi, Kenya ambapo baada ya tukio hilo la kigaidi, Al-Shabaab walikusanyika Eneo la Barawa mjini huko Sudan kisha wakaangusha bonge la pati kupongezana kwa mauaji hayo ya zaidi ya watu 60. SASA ENDELEA…

Baada ya tukio hilo, kuliibuka taarifa kuwa kulikuwa na Mtanzania alikutwa na dhahama hiyo hivyo ilibidi Jeshi la Polisi la Tanzania kufuatilia huku kukiwa na taarifa za vitisho za Al-Shabaab.Baadaye jeshi hilo liligundua kuwa Mtanzania aliyekuwepo kwenye shambulio hilo ni Vedasto Nsanzugwanko ambaye alinusurika lakini akiwa amejeruhiwa vibaya.

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba (kwa sasa amestaafu) alisema kuwa jeshi hilo lilifuatilia kwa undani taarifa zilizozagaa katika mitandao ya kijamii kwamba Kundi la Al-Shabaab lilikuwa likijipanga kuishambulia Tanzania na Uganda.

DCI Manumba alikiri kusikia taarifa hizo na kusema kuwa Jeshi la Polisi la Tanzania lilikwishaanza kufanya uchunguzi wa kina. Alikaririwa: “Siwezi kueleza ni uchunguzi wa aina gani tutakaofanya, hiyo ni siri yetu.”
Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), Meja Eric Komba alisema kuwa kuna uwezekano taarifa hizo zikapikwa na wajanja wachache kwa ajili ya kuwajengea hofu wananchi.

Naye alikaririwa: “Taarifa za kwenye mitandao wakati mwingine ni uzushi mtupu… kuna kipindi ziliwekwa taarifa za uongo zinazohusu kundi hilo.”Wakati jeshi hilo likijiimarisha, Nsanzugwako ambaye ni Meneja wa Kitengo cha Kulinda Watoto kwenye Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Watoto (Unicef), Kenya alikuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Aga Khan, Nairobi.

Kwa mujibu wa Nsanzugwako, alikuwa akitokea kazini akapitia kwenye jengo hilo ili walau apate kahawa lakini alishtuka alipopigwa risasi miguu yote miwili kisha kufuatiwa na purukushani kubwa.Nsanzugwako alianza kukimbia na wenzake huku wakijaribu kuokoa watoto waliokuwepo katika eneo hilo ambao walikuwa katika shindano la mapishi lililoandaliwa na Radio Africa Group.

Watoto nao walikuwa wakikimbia ovyo wakipanda ghorofa za juu zaidi na magaidi nao walianza kuwafuata.
Magaidi hao walikuwa wakikimbiza watu ambapo na Nsanzugwako alikutana nao uso kwa uso ambao walimfyatulia risasi kabla ya kufanikiwa kujiokoa na kukimbizwa hospitalini hapo na waokoaji.

Baadaye kuliibuka taarifa kwamba, kumbe kwenye tukio hilo mpwa wa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta anayejulikana kwa jina moja la Mbugua alikwenda na mchumba wake, Rosemary katika jengo hilo kununua pete za ndoa kwa ajili ya maandalizi ya harusi yao.

Kwa mujibu wa mashuhuda, Mbugua alikuwa ameshatoka nje baada ya magaidi hao kuishambulia Westgate Mall ndipo aliamua kurudi ndani kumuokoa mchumba wake ambapo alikutana na magaidi hao ambao walimshambulia kisha akapoteza maisha papohapo.

Je, nini kitaendelea? Usikose wiki ijayo.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.