Nicodemus Jonas, Dar es Salaam
IKIWA ni siku moja tu kabla ya
pazia la Ligi Kuu Bara kufunguliwa, lile agizo la Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), kupitia rais wake, Jamal Malinzi kwa klabu zote zenye
wachezaji wa kimataifa kuhakikisha zinawalipia dola 2,000 (Sh milioni 4)
kila mmoja limechukua sura mpya, baada ya kubainika Simba pekee ndiyo
iliyotekeleza agizo hilo.
Simba imetekeleza agizo hilo licha ya awali kuwa kwenye makubaliano na klabu nyingine za Yanga na Azam FC kugomea mpango huo. Klabu hizo zilikuwa katika mpango wa kugomea kulipia kiasi hicho cha fedha mpaka zitakapozungumza kisha kutoa tamko, lakini taarifa za uhakika zilizopatikana jana, Simba wamepita chinichini na kulipa.
Awali, Malinzi alitamka kwa msisitizo kuwa klabu ambazo hazitalipa ada hiyo kwa wachezaji wake hao, basi hawatapata kibali cha kucheza soka nchini katika mechi za kimashindano.
Akizungumzia sakata hilo, Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa alifunguka kuwa, lazima kila klabu itekeleze agizo hilo kwa kuwa ni kanuni iliyopitishwa na Kamati ya Utendaji ya TFF kwa ajili ya msimu huu utakaoanza rasmi kesho Jumamosi.
“Suala la klabu kutuandikia barua kupinga ada hiyo nimekuwa nikilisikia kwenye vyombo vya habari, sina taarifa rasmi kuhusu ombi hilo. Halafu suala hili lipo kikanuni, limepitishwa na Kamati ya Utendaji ya TFF, hiyo haina mjadala lazima litekelezwe,” alisema katibu huyo wa zamani wa Yanga.
“Niwapongeze Simba kwa muitikio wao katika jambo hili, naweza kusema mpaka sasa (jana) wao ndiyo wametekeleza agizo lililotolewa na rais.
“Jana (juzi) na leo (jana) kamati ya sheria ilikuwa na vikao kupitia majina ya wachezaji wanaostahili kuchezea ligi kuu, pengine hao wengine tusubiri majina yakitoka ndipo tutajua nani anafaa na nani hafai kulingana na sheria zetu,” alimaliza Mwesigwa.
Baadhi ya wachezaji wa kimataifa wa Yanga ni Donald Ngoma, Haruna Niyonzima, Twite, Amissi Tambwe, Thaban Kamusoko na Coutinho.
Wakati gazeti hili likiingia mitamboni Msemaji wa Azam FC, Jaffar Maganga alisema klabu yao imekubali kulipa gharama hizo licha ya kuwa wanaamini siyo sawa. Yanga wao mpaka jana walikuwa hawajalipa fedha hizo.

Note: Only a member of this blog may post a comment.