Steve Nyerere akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani).
Staa wa filamu za Kibongo, Wema Sepetu na wasanii wenzake wa kike leo wamezindua Kampeni ya ‘Mama Sema na Mwanao’ ambayo itafanya tamasha kubwa lenye lengo la kuongea na vijana na litazunguka mikoa kumi ya Tanzania kwa ajili ya kuamsha vijana ikiwa ni moja ya sera za Chama Cha Mapinduzi ‘CCM’. Akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Protea, Wema alisema lengo la kampeni hiyo ni kuhamasisha vijana na kuongea nao kama akinamama ili kuachana na dhamira potofu na kulinda amani ya nchi ambayo inaonekana kuanza kupotea kwa vikundi vidogovidogo.
“Tumeamua kuunda timu ya akinamama ambapo itakuwa chini ya Mama Salma Kikwete na Mama Magufuli na tutazunguka mikoa kumi na kuongea na vijana wote, hii ni sehemu pia ya kuhamasisha watu kuchagua mtu mchapa kazi na tuna asilimia tisini na tisa ya ushindi, akina mama tunaweza kupaza sauti zetu kwa pamoja ili kuwaelimisha vijana,” alisema Wema.
Naye Steve Nyerere akiwa kama mwenyekiti wa kundi hilo alisema kuwa wameamua kuwatumia akinamama kwenye hilo kwa sababu wao wakisema wanasikika kutokana na ujasiri na uwezo waliopewa na Mungu.
“Akinamama wana uwezo wa kuongea na mpenzi, kuongea na rafiki, kuongea na watoto wao kwa sababu Mungu amewapa kipaji, hii imekuwa ni fursa kwao ili kuwafikia watoto wao na vijana wote wa Tanzania,” alisema Steve Nyerere.
Wasanii watakaokuwa kwenye msafara huo ni Wema Sepetu, Halima Yahya ‘Davina’, Fatuma Makongoro ‘Bi Mwenda’, Wastara Juma, Salome Urassa ‘Tea’, Harriety Chumila, Sabrina Rupia ‘Caty’, Mama Nyamayao, Snura Mushi, Mama Rolaa, Wellu Sengo na Yobnesh Yusuph ‘Batuli’.
(Habari/Picha: Hamida Hassan na Imelda Mtema)

Note: Only a member of this blog may post a comment.