NIMEWAHI kusema
huko nyuma kuwa moja kati ya vitu vinavyoturudisha sana nyuma sisi watu
weusi, ni wivu, hasa wa kijinga. Wivu ni tabia kama zilivyo tabia
nyingine, mtu huzaliwa nayo, ingawa wachache hujifunza ukubwani, wengi
kati yao wakiwa ni tegemezi!
Mtu anayejimudu mara nyingi hatawaliwi
na wivu, labda uwe wa maendeleo, ambao pia sisi watu weusi tumekosa.
Maisha ya aina hii yapo sana katika jamii yetu, mmoja kumchukia mwenzake
bila hata sababu za msingi, maana hata ukimuita na kumuuliza chanzo cha
yote hayo, hukosa cha kusema.
Nimeanza hivi baada ya kuchukizwa na
tabia ya mtu mmoja huko kwenye mitandao ya kijamii, Instagram,
anayejiita King Lawrence, ambaye kwa muda mrefu, amekuwa akimuandama
sana Zarinah Hassan ‘Zari’ binti raia wa Uganda aliyezaa na nyota wa
Bongo Fleva, Diamond Platinumz.
Simfahamu yeyote kati yao kwa maana ya kukutana au kuzungumza, lakini nazipata habari zao kupitia mitandao na magazeti ya hapa nyumbani na kule Uganda. Inaelezwa kabla ya Zari kudondokea mikononi mwa Diamond, alikuwa akiishi na rafiki wa King Lawrence, Ivan ambaye alizaa naye watoto watatu.
King analalamika sana mitandaoni kuliko Ivan mwenyewe na amekuwa akitoa maneno mengi ya kejeli, dharau na hata matusi kwa shemeji yake na Diamond pia.
Kilichonisikitisha zaidi, ni ingizo lake la hivi karibuni (post mtandaoni) akidai kumwandikia barua Zari ili mtoto wake akachukuliwe vipimo vya kutambua vinasaba (DNA) kwani ana hofu mtoto huyo ni wake yeye (King).
Siku chache zilizopita, akitoa madai hayohayo, alisema mtoto huyo ni wa Ivan, kwani mahesabu yanaonesha asingeweza kujifungua Agosti halafu ujauzito uwe wa Diamond.
Huyu jamaa ni limbukeni. Eti amekomaa kwamba yeye alilala na Zari, hivyo Latifa ni mwanaye. Naambiwa huyu King ni mpambe mkubwa wa mzazi mwenzake na Zari. Sasa unajiuliza, hivi mtu mwenye akili timamu, anaweza kutoa madai kama haya mchana kweupe? Kwamba alilala na shemeji yake?
Nadhani jamaa ana matatizo na wivu wa kijinga uliopindukia. Anaonekana kuchukizwa sana na kitendo cha Zari kuwa na Diamond, maana mfululizo wa maneno yake hayaoneshi kama mtu anayemtakia mema shemeji yake.
Kijana wa kiume unakuwaje na wivu wa namna hiyo kwa mwanamke? Tumezoea hali hiyo wanakuwa nayo wadada, lakini mwanaume siku zote ni mtu wa kupigana ili kupiga hatua kutoka pale alipo.
Unapochukua muda mwingi kumzungumzia mtu, tena mwanamke, unawapa watu mashaka juu ya uwezo wako, kwanza kiakili na pia kiuchumi. Tumezoea kuwaona wapambe wakifanya vitu kwa kujipendekeza kama hivi na kijana wa kiume unapofikia hatua hii, lazima ujihesabu kama umefeli.
Nimshauri King Lawrence, aachane na Zari kwa sababu anajiabisha, kwanza yeye kama mwanaume, lakini pia kama rafiki wa karibu wa Ivan. Anamtukana mwanamke ambaye amemzalia mtu ambaye yeye anajipendekeza. Hivi hafikirii jinsi gani watoto wa Zari wanavyomuona, au anadhani wanaweza kumchukia mama yao kupitia yeye?
Kama anafanya hivyo anavyofanya kwa sababu ameumizwa sana na mwanamke huyo kuzaa na Diamond, nadhani angetuliza tu mzuka, kwa sababu maisha ndivyo yalivyo na hana la kufanya na kama anatumwa na Ivan afanye hivyo anavyofanya, basi ni tatizo kubwa zaidi kwake.
Mtoto wa kiume siku zote anapaswa kutumia akili na nguvu zake kutafuta maisha yake, kwa sababu mtegemea cha ndugu hufa maskini.


Note: Only a member of this blog may post a comment.