Akizungumza na gazeti hili, Katibu wa CCM Wilaya ya Ilala, Ernest Challe alisema baadhi ya wagombea ambao hawakukubaliana na matokeo yaliyotangazwa hivi karibuni, wameanza kuwasilisha barua za pingamizi.
“Tumeanza kupokea barua za pingamizi kutoka kwa baadhi ya wagombea ambao hawakuridhika na matokeao ya uchaguzi uliofanyika kutafuta wawakilishi wa kukiwakilisha chama katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu,” alisema Challe.
Challe alisema kuwasilishwa kwa barua hizo za pingamizi ni moja ya taratibu za chama, ambazo zinamtaka mwanachama yeyote ambaye hajaridhika na maamuzi au matokeo, kuwasilisha malalamiko kwa njia ya maandishi.
Katika kata ya Buguruni, waliowasilisha barua za kupinga matokeo ya udiwani katika kata hiyo ni wagombea wawili ambao ni Barua Mwakilanga na Magina Lusungule. Akizungumzia uwasilishaji wa barua hizo, Kaimu Katibu CCM kata ya Buguruni, Abdu Kinong’ozi alisema kuwa kutokana na mgogoro uliotokea hivi karibuni kwa baadhi ya wagombea kupinga matokeo ya udiwani, wagombea wawili wamewasilisha barua za pingamizi.
“Hadi hivi sasa tumeshapokea barua za wagombea wawili ambao hawakukubaliana na matokeo ya udiwani yaliyotangazwa hivi karibuni kwa kudai kuwa uchaguzi huo uligubikwa na udanganyifu,” alisema Kinong’ozi. Kwa mujibu wa Kinong’ozi, baada ya kuwasilishwa kwa barua hizo, watakaa kikao kujadili malalamiko hayo na kuyatolea ufafanuzi.

Note: Only a member of this blog may post a comment.