Thursday, August 6, 2015

Anonymous

ACT WAMTUMIA MWIGAMBA KUJARIBU KUTIA KITUMBUA CHA CHADEMA MCHANGA!

Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Samson Mwigamba.
Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Samson Mwigamba (pichani), amechukua fomu ya kugombea ubunge katika Jimbo la Ubungo ambako atapambana na Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Didas Masaburi wa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Said Kubenea wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Mwigamba ameahidi kuwa endapo atapata nafasi ya kuwa mbunge, atahakikisha sheria inayowabana wabunge wasio watendaji inapitishwa bungeni ikiwa ni pamoja na wananchi kuwa na mamlaka ya kumtengua mbunge kabla ya kipindi chake kumalizika.

Mwigamba alichukua fomu hiyo jana jijini Dar es Salaam, katika Ofisi za jimbo zilizopo Ubungo External na kusema kuwa azma yake ya kuwania nafasi hiyo ni kuwapatia wananchi wa jimbo hilo maendeleo waliyoyakosa kwa muda mrefu.

Alisema moja ya changamoto kubwa iliyopo katika jimbo hilo ni tatizo la maji ambalo Mbunge aliyepita alishindwa kulitatua, John Mnyika (Chadema), pamoja na tatizo la foleni katika eneo la Ubungo ambako ni kitovu cha jijini hili.

“Naamini kupitia ACT-Wazalendo tunaweza kuwapatia maendeleo wananchi wa jimbo la Ubungo ambayo wameyakosa kwa vipindi vyote walivyokuwapo wabunge waliotangulia pamoja na kutatua kero mbalimbali,” alisema Mwigamba.

Pia, alisema kuwa kupitia ilani ya chama chake, hawawezi kukiuka taratibu na kanuni za katiba hiyo, hivyo watawatumikia vyema Watanzania kwa kuzingatia hayo bila kubadilisha misimamo waliyojiwekea kama vyama vingine.

Kwa mujibu wa Katibu wa Jimbo hilo, Patrick Malya, waliochukua fomu hadi jana ni 11 na waliorudisha ni wagombea nane na kwamba kura za maoni zinatarajiwa kufanyika Jumamosi wiki hii.

Pia waliorudisha fomu katika Ofisi hizo jana kwa ajili ya kuwania ubunge katika jimbo la Kibamba ni mwandishi wa habari wa gazeti la The Guardian, Dickson Ng’ili na Eliya Msope ambaye ni mwenye ulemavu wa macho.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.