Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza
ameapishwa hii leo, siku sita kabla ya tarehe rasmi kuambatana na katiba
ya nchi hiyo ambapo alitarajiwa kuapishwa mnamo tarehe 26 mwezi Agosti.
Taarifa kutoka ofisi ya Rais imesema
Nkurunziza ameapishwa rasmi hii leo kuwa rais wa nchi hiyo kwa muhula
mpya wa miaka mitano ijayo. Sherehe hiyo ya kuapishwa kwa kiongozi huyo
wa Burundi imekuja ghafla na kutangazwa saa chache kabla ya sherehe
yenyewe kufanyika.
Maofisa wa kijeshi wameagizwa leo asubuhi kuvalia sare zao rasmi na kufika bungeni kwa ajili ya sherehe hizo za ghafla za kuapishwa kwa Rais Nkurunziza. Hakuna viongozi kutoka nchi za kigeni ambao wamealikwa kuhudhuria sherehe hizo za kuapishwa kwa kiongozi huyo wa Burundi.
Muhula wa tatu wa Nkurunziza
umesababisha ghasia nyingi, kwa mujibu wa katiba ya Burundi, rais
anastahili kukaa madarakani mihula miwili tu ya miaka mitano kila
mitano, lakini Nkurunziza na washirika wake wamedai muhula wake wa
kwanza madarakani, alichaguliwa na bunge na sio umma na kwa hivyo
anastahili kuendelea kuwa madarakani.
Uamuzi wake mwezi Aprili mwaka huu kuwa
atagombea muhula wa tatu madarakani umezua mzozo mkubwa wa kisiasa na
kusababisha ghasia nchini humo.
Nkurunziza alishinda muhula wa tatu
baada ya uchaguzi wa rais uliofanywa tarehe 21 mwezi Julai ambao
ulisusiwa na vyama vya upinzani nchini humo na mapema mwezi huu
alitangazwa na tume ya uchaguzi nchini Burundi CENI kuwa mshindi kwa
asilimi sitini na tisa ya kura zilizopigwa dhidi ya mpinzani wake wa
karibu Agathon Rwasa ambaye licha ya kuususia uchaguzi huo alipata
asilimi 18 ya kura zilizopigwa.
Baraza la usalama la umoja wa Mataifa
limeelezea wasiwasi wake kuhusu hali ya kisiasa na kiusalama katika
taifa hilo dogo la Afrika Mashariki na kutoa wito pande zĂnazozana
Burundi kufanya mazungumzo ili kuutatua mzozo huo na kuepusha taifa hilo
kutumbukia katika vita.
Watu kadhaa mashuhuri nchini humo
wametorokea nchiza kigeni wakihofia usalama wao na wengine waliosalia
nchini humo wamelengwa kwa kuuawa, kushambuliwa, kukamatwa, kuteswa au
kutishiwa maisha yao wakiwemo maafisa wa kijeshi,wanahabari na
wanaharakati wa kutetea haki za binadamu.
Milio ya raisasi imekuwa ikisikika
karibu kila siku katika mitaa ya mji mkuu wa Burundi, Bujumbura huku
askari na wanajeshi wakijaribu kuwakandamiza wanaompinga Rais
Nkurunziza.
Mzozo huo wa Burundi unahofiwa kuwa
huenda ukalitumbukiza taifa hilo tena katika vita vya wenyewe kwa
wenyewe kama vilivyoshuhudiwa kati ya mwaka 1993 hadi mwaka 2006 ambapo
kiasi ya watu laki tatu waliuawa.
Umoja wa Mataifa umewasajili maelfu ya
wakimbizi kutoka Burundi katika nchi jirani za Rwanda,Tanzania, Jamhuri
ya kidemokrasia ya Congo na Uganda tangu mzozo huo uanze.
NA DW

Note: Only a member of this blog may post a comment.