ASALAMALEIKUM
ndugu zangu Waislamu ambao mpo ndani ya mfungu wa Mwezi Mtukufu wa
Ramadhan. Bila shaka shaka swaumu inapanda na ishallah Mungu atawafanyia
wepesi mtaumaliza mwezi huu salama.
Wameona sera zao haziendani, wakaamua kuachana. Kila mmoja anaanza kutafuta pumziko lingine kwa muda wake.
Lakini wakati hayo yakiendelea, kuna mmoja kati ya wawili hao anakuwa ameguswa na ugomvi wao.
Anataka kurejesha penzi, hajui ataanzia wapi. Huyo ndiye ninayezungumza naye leo hapa.
Vipo vitu vya msingi vya kutafakari kabla hujaamua kufufua penzi lililokufa, ni vyema ukajifunza:
JITATHMINI
Kabla hujaamua kufufua penzi lililokufa kwanza unapaswa kujitathmini juu ya penzi lako la awali na sababu ya kuachana kwenu. Jiulize ni nini kilisababisha hadi mkafikia hatua ya kuachana?
Pima uzito wa sababu hizo za kuachana kabla ya kuamua kuomba nafasi upya. Sababu hiyo inaweza kubadilika au haiwezekani? Usije ukawa sababu ya kuachana kwenu ni mwenzako kukwambia anaolewa na mtu mwingine halafu wewe ukaendelea kulazimisha kuomba nafasi.
Sababu ya kuachana kwenu ikiwa ni ya yeye kupata bwana wa kumuoa na mipango tayari imeshafika patamu, huna haja ya kuendelea kurejesha penzi hilo maana tayari linakuwa limeshafika hatua ambayo huwezi kulizuia.
Jiulize nani alikuwa chanzo cha mgogoro? Chanzo chake ni nini? Ukishagundua chanzo chake na nani alikuwa anasababisha, anza kutafuta suluhu kwanza moyoni mwako.
Jitathmini kama chanzo kilikuwa ni tabia yako wewe labda mfano hasira, jiulize unaweza kubadilika? Ufanyeje ili uweze kubadilika? Ukishabadilika, hauwezi kurudia tena tabia hiyo?
Hakikisha kwanza unajishughulikia matatizo yako. Katika maeneo yote ambayo wewe ulihusika, hakikisha unajisahihisha mwenyewe ndipo baadaye utamshirikisha mwenzako pindi utakapokuwa umekutana naye kwa ajili ya mazungumzo.
TAZAMA VIKWAZO
Wakati unatafuta muda wa kukutana na mwenzi wako, jiulize kwa wakati huo ana kikwazo gani? Yawezekana wakati mnaachana hakuwa na kikwazo lakini wakati unataka kurejesha penzi, unakuta mwenzako ana kikwazo.
Hawezi kurudiana na wewe wakati huo tayari yupo katika mikakati ya kufunga ndoa na mtu. Au yupo na mtu ambaye tayari wameendana, wameshatambulishana kwa wazazi na kuweka mikakati ya ndoa.
ANDAA SULUHU
Ukishabaini chanzo, sababu na kujiridhisha kwamba umeshafanyia kazi upungufu wako, omba nafasi ya kukutana na mwenzi wako. Ikiwezekana watumie hata watu wake wa karibu ili wakusaidie kukukutanisha naye.
Muombe radhi. Mueleze kwamba umeshayafanyia kazi matatizo yako. Umebaini tatizo na uko tayari kwa suluhu. Hata katika maeneo ambayo yeye alikuwa akikosea, tumia lugha nzuri kumueleza namna ambavyo anapaswa na yeye kubadilika ili msijikute mnaingia tena kwenye migogoro.
Usimlamu. Onesha dhamira ya dhati ya kutaka kuishi kama zamani. Mpe nafasi pia akueleze vitu ambavyo pengine ulikuwa unamkwaza. Vikubali na ahidi kuvifanyia kazi.
Akikuelewa, ongeza upendo maradufu. Ishi kwa kujikumbusha kila siku maeneo ambayo ulikuwa unayakosea. Usirudie makosa. Hakika mtaheshimiana na mtafurahia penzi lenu na kila mmoja akihofia kumuudhi mwenzake.
Mara nyingi penzi lililokufa likifufuka huwa linakuwa tamu, linakuwa na matokeo mazuri zaidi ya lile la awali.
Ni matumaini yangu mtakuwa mmenielewa, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.


Note: Only a member of this blog may post a comment.