Wednesday, May 13, 2015

Anonymous

WEWE NI RAFIKI WA AINA GANI?

Ukipenda usipende rafiki zako wamekuweka katika kundi fulani, unaweza kuwa na mtu ambaye rafiki zako wanakukumbuka kila mara kwa kukutakia mema, au unaweza kuwa aina ya rafiki ambaye rafiki zako wakikuona tu wanaanza kukutukana na kukulaani. Sasa wewe unajijua rafiki zako wamekuweka kundi gani?

Inawezekana wewe ni aina ya rafiki ambaye unakumbukwa tu kama kukiwa na mnuso au watu wanataka kutoka out, hasa kama una pesa au gari, lakini kama hakuna ishu hakuna anayekutafuta. Au wewe ni aina ya rafiki ambaye watu wakiishiwa ndiyo wanakukumbuka? Maana una uwezo wa kumkopesha mtu hata akipiga simu saa nane za usiku, bila matatizo unamtumia hela tu, halafu uzuri wake wewe huwa hudai kiviiile.

Halafu kizuri zaidi siku za sikukuu unawakaribisha wote unaowadai kwa bonge ya mnuso, tena kiroho safi. Au wewe ni yule rafiki ambaye akiombwa mchango, hata ile michango ya kiajabu ya kisiku hizi inayosema mchango si chini ya laki we unatuma tu, halafu kwenda shughuli huendi? Au wewe ndiyo wale marafiki ambao kamwe hawachangii mchango wowote, hata kama unamsaidia?

Au wewe ndiye aina ya rafiki ambaye ukisikia mwenzio ana shida lazima uhangaike kumsaidia, hata kama ukisikia yuko gerezani Uchina utaenda tu kujaribu kumtoa? Yaani aina ya wale tunaowaita marafiki wa ukweli? Tatizo ni kuwa marafiki wa dizaini hii wako wachache sana.

Au wewe ndiye wale marafiki ambao hawana doa, wana kazi nzuri, nyumba nzuri, wanavaa vizuri, wana stori nzuri, wana roho nzuri, yaani mpaka wenzio wanataka kuwa karibu na wewe kila mara?

Au wewe ndiye yule rafiki ambaye wenzako wanakufanya kichwa cha habari kila wakikutana? Kazi yao kukuongelea wewe tu na vituko vyako, ulivyofumaniwa huku, ulivyoiba kule, ulivyofukuzwa kazi mwaka juzi, yaani wewe ndiye chachu ya mazungumzo?
Au wewe ndiye yule rafiki anaedai anamjua kila mtu? Ukiulizwa kuhusu Ikulu, kuna mtu unamjua, TRA kuna mtu unajua na sehemu zingine nyeti una watu unaowajua.

Au wewe ni aina ya rafiki ambaye ukimuona rafiki yako yoyote lazima umpige mzinga hata kama una fedha? Wewe ni rafiki wa aina gani? Tukutane www.johnkitime.co.tz

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.