Martha Mboma na Wilbert Molandi
BAADA ya kusaini mkataba wa miaka mitano na klabu yake mpya ya Sonderjyske ya nchini Denmark, aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, Mganda, Emmanuel Okwi, amefunguka kuwa anaishukuru klabu yake hiyo ya zamani. Okwi amewatumia Simba waraka wa kuwashukuru lakini pia akimshukuru kocha wake wa sasa, Jakob Michelsen, ambaye alimfuatilia kwenye michezo 20 kabla hajampa nafasi.
Okwi amefanikiwa kuuzwa nchini humo mapema mwezi huu mara baada ya kufuzu vipimo vya afya.
Okwi amefunguka hayo kupitia ukurasa wa Mtandao wa Twitter kwa kuwashukuru mashabiki wa Simba na Waganda kwa kuweza kumsapoti na kufanikiwa kucheza soka la kulipwa Ulaya. “Napenda kuwaambia rasmi kuwa nimejiunga na Klabu ya Sonderjyske kwa muda wa miaka mitano na napenda kumshukuru kocha, Jakob Michelsen ambaye alikuwa akinifuatilia kwenye michezo 20 na kuweza kuvutiwa na uwezo wangu.
“Shukrani zangu za dhati ziende kwa Klabu ya Simba kwa mchango wao mkubwa kwangu na kuweza kufika hapa nilipo sasa bila kuwasahau mashabiki wangu wa timu ya taifa ya Uganda na mashabiki wangu wote kwa jumla. Ninapata meseji zenu na simu, lakini nashindwa kuwajibu wote, tambueni niko pamoja nanyi na nawapenda.
“Nitapambana huku Ulaya kuhakikisha naweza kuinufaisha klabu yangu japo nafahamu wazi na kupambana na changamoto mpya,” aliandika Okwi.
Michelsen aliwahi kuwa kocha wa vijana wa timu ya taifa pamoja na kocha msaidizi wa Taifa Stars.

Note: Only a member of this blog may post a comment.