HII ni wiki ya pili sasa kikosi cha Simba kimepiga kambi Lushoto, Tanga kikijiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu Bara ambapo kila siku zinavyozidi kwenda ndiyo mabadiliko yanavyoonekana.
Awali, wachezaji walikuwa wakiilalamikia hali ya hewa ya baridi kali iliyopo maeneo haya, lakini imekuwa tofauti kwa sasa kutokana na kila mmoja kuifurahia.Championi ambalo limepiga kambi karibu na uwanja wanaofanyia mazoezi Simba, limekuwa likiwashuhudia wachezaji wa kikosi hicho wakiendelea kujifua huku na kila siku wakionekana kuyafurahia mazoezi ya kocha mkuu, Dylan Kerr pamoja na kocha wa viungo, Dusan Momcilovic.
Ikumbukwe kuwa, wakati Simba inaanza mazoezi wiki moja nyuma, kila mchezaji alikuwa akilalamika kwamba huku walipo sipo kutokana na kushindwa kuhimili baridi lakini ukiwauliza kwa sasa wanakwambia wanatamani kubaki kwa muda zaidi.
Imekuwa kawaida kwa kikosi hicho kuchukua takriban saa mbili kwenye mazoezi lakini jana kilifanya kwa saa moja, tena wachezaji wakinyoosha sana viungo kuliko kuuchezea mpira.
Kwa jinsi Kerr anavyowaandaa wachezaji wake, ni wazi kabisa msimu ujao wa ligi kuu, timu hiyo itakuwa na vikosi zaidi ya viwili vya uhakika kutokana na kocha huyo kuumiza kichwa kila siku kutengeneza pacha nyingi.
Pacha ambayo imeonekana kuiva kisawasawa ni ya washambuliaji Mganda, Hamis Kiiza na Elius Maguri bila ya kuisahau ile ya Mussa Hassan Mgosi na Ibrahim Ajib.
Kwa upande wa mabeki wa kati, tayari Mohammed Fakhi na Juuko Murushid wanaonekana kuelewana sana huku ikiandaliwa nyingine ya Hassan Isihaka na Juuko.

Note: Only a member of this blog may post a comment.