Wilbert Molandi,
Dar es SalaamMSHAMBULIAJI wa
Yanga, Mrundi, Amissi Tambwe, amethibitisha kuwa yeye ni hatari kwa
mipira ya vichwa baada ya kupiga vichwa vinne ndani ya dakika 90 huku
akifunga bao.
Mrundi huyo aliyekuwa mfungaji bora wa msimu wa 2013/2014 akipachika mabao 19, alipiga vichwa hivyo wakati timu hiyo ilipovaana na Kombaini ya Majeshi katika mchezo uliomalizika kwa Yanga kushinda mabao 3-0. Katika msimu uliopita wa ligi kuu, mshambuliaji huyo alifanikiwa kufunga mabao 14 huku idadi kubwa ya mabao akifunga kwa njia ya kichwa.
Katika mechi hiyo, Tambwe aliifungia timu yake bao la pili kwa kichwa akiunganisha mpira wa krosi uliopigwa na Simon Msuva wakati mechi hiyo ikiendelea.
Mara baada ya kufunga bao hilo kwa kichwa, akapiga kichwa kingine katika dakika ya 45, kabla ya mpira kudakwa na kipa wa Kombaini ya Majeshi.
Baada ya dakika tano, mshambuliaji huyo akapiga kichwa kingine ambacho alifunga bao lililokataliwa na mwamuzi wa kati akidai kuwa alimsukuma kipa wakati anafunga kabla ya kulilalamikia bao hilo.
Katika dakika ya 70, mshambuliaji huyo alipiga kichwa kingine cha nne kilichogonga mwamba na kutoka nje.
Katika mechi hiyo, wafungaji wa mabao mengine mawili ni Simon Msuva aliyefunga bao la kwanza na Mzimbabwe, Donald Ngoma.


Note: Only a member of this blog may post a comment.