Monday, June 15, 2015

Anonymous

SIMON MSUVA Aeleza Kilichotokea SAUZ

Wilbert Molandi Dar es Salaam
MUDA mfupi baada ya kurejea nchini akitokea Afrika Kusini kufanya majaribio, kiungo mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva, ameeleza kila kitu kilichotokea nchini humo.

Kiungo huyo ambaye inadaiwa aliutoroka uongozi wa Yanga, alitimkia Afrika Kusini ‘Sauz’ Jumatano iliyopita na alifanya majaribio ya siku tatu katika kikosi cha Bidvest Wits kinachoshika nafasi tatu kwenye ligi kuu ya nchi hiyo. Alirejea nchini juzi Jumamosi saa saba mchana.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Msuva alisema kuwa bado hajapewa majibu rasmi ya majaribio yake ya siku tatu aliyoyafanya akiwa na timu hiyo akasisitiza anatarajia kuyapata hivi karibuni baada ya menejimenti ya Bidvest kukutana. Msuva alisema akiwa kwenye majaribio hayo, amejifunza vitu vingi vya ndani na nje ya uwanja kupitia kwa wachezaji wakongwe kama Mzambia, Chris Katongo.

Alisema alichojifunza kutoka kwa wachezaji wa Wits ni aina ya uchezaji kutoka kwa washambuliaji wake ambao ni nadra kupoteza nafasi za kufunga wakiwa ndani ya 18.

“Nimerejea jana (Jumamosi) mchana nikiwa na malaria nikitokea Afrika Kusini nilipokwenda kwenye majaribio ya siku tatu, ninashukuru nilifanya vizuri binafsi, lakini ninasubiri majibu kutoka kwa wakala wangu wa hapa atakayepata kutoka kwa wakala wangu anayeishi nchini huko.

“Siwezi kusema moja kwa moja kuwa lini nitayapata, hivyo nasubiri kwanza, ninashukuru kwa siku hizo tatu nilizofanya majaribio, nimefunza vitu vingi.“Washambuliaji wa Wits akiwemo Katongo wenyewe hawapendi na hawataki kabisa kupoteza nafasi za kufunga mabao wanazozipata ndani ya uwanja kwa kuanzia mazoezini hadi kwenye mechi.

“Pia wachezaji wa Wits wengi wapo vizuri kifedha, hiyo ni kutokana na mshahara mzuri wanaolipwa. Hilo ni suala la viongozi wetu kuiga,” alisema Msuva. Naye Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha, amesema wamepata taarifa kuwa kiungo huyo amefuzu lakini akasisitiza watampeleka kwenye kamati ya maadili ya timu hiyo kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu kutokana na kutoroka.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.