KIUNGO Haruna Chanongo aliyeitwa katika kikosi cha Taifa Stars kujiandaa na mechi za kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika 2017, jana Ijumaa alitengwa katika mazoezi ya timu hiyo yaliyosimamiwa na Kocha Mart Nooij.
Wakati Chanongo akitengwa kwenye mazoezi hayo, Azam FC imesema haina mpango na mchezaji huyo licha ya kupiga picha akiwa amevaa jezi ya timu hiyo ambayo ilisambaa katika mitandao ya kijamii juzi usiku.
Chanongo alitinga katika mazoezi hayo Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam lakini mtaalamu wa viungo wa Taifa Stars, Joakim Mshanga alimtaka kutofanya mazoezi ya pamoja na wenzake kutokana na kusumbuliwa na kifundo cha mguu.
Championi Jumamosi lilikuwepo mazoezini na kumshuhudia Chanongo akiamuriwa kuvaa raba za kawaida badala ya vile vingine vya mazoezi vya kawaida kisha akawa anafanya mazoezi mepesi chini ya uangalizi wa Mshanga na Nooij.
Chanongo alitumia dakika 60 akifanya mazoezi ya kutembea huku Nooij akimsisitizia kutokimbia ili kuwezesha jeraha lake kupona haraka. Taifa Stars itacheza na Misri Juni 13 au 14, mwaka huu kufuzu Afcon 2017.
Pia habari zinasema aliyekuwa Kocha wa Mtibwa Sugar, Mecky Maxime amepewa shavu Taifa Stars kuwa kocha msaidizi.
Wakati huohuo, kuhusu Chanongo kupiga picha akiwa na jezi ya Azam na kuhusishwa na usajili kwa timu hiyo, Katibu Mkuu wa timu hiyo, Idriss Nassor alisema: “Huyo kajifurahisha tu, hayupo katika hesabu zetu kabisa.”
Note: Only a member of this blog may post a comment.