Saturday, May 30, 2015

Anonymous

TFF yamzuia straika mpya YANGA SC

Mshambuliaji Donald Ngoma.
Sweetbert lukonge Dar es Salaam.
UONGOZI wa FC Platinum ya Zimbabwe umesema umekubaliana na Yanga iweke fungu la dola 250,000 (Sh milioni 508) mezani ili mshambuliaji Donald Ngoma atue Jangwani.Yanga kuonyesha jeuri ya fedha, imesema iko tayari kumwaga fedha hizo kwenye akaunti ya FC Platinum lakini hofu ni kuhusiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambalo linasababisha mchezaji huyo ashindwe kufika jijini Dar es Salaam.

Ofisa mmoja wa FC Platinum aliyesema anazungumza kwa niaba wa mwenyekiti wa klabu hiyo, Dumisani Sisale, ameliambia Championi Jumamosi kuwa, wamekubaliana na Yanga dau hilo la dola 250,000. “Sisi bado tunamhitaji Ngoma, tunataka kufanya vizuri kimataifa msimu ujao. Lakini Yanga wamesisitiza wako tayari kutoa fedha hizo na sisi tumesema tutamwachia.

“Lakini juzi, wametupigia simu wakieleza kwamba wanalazimika kusubiri kuona kama shirikisho lenu (Tanzania) litaongeza nafasi ya wachezaji wa kigeni. Wametueleza ni wachezaji watano tu hadi sasa wanaruhusiwa kusajiliwa,” alisema ofisa huyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Joseph.

Gazeti hili lilifanya uchunguzi ndani ya Yanga na kuelezewa kwamba awali Yanga ilituma tiketi lakini Ngoma akawa amebanwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Zimbabwe kilichokuwa nchini Afrika Kusini kushiriki mashindano ya Cosafa.

“Lakini sasa uongozi umemuambia asubiri kwanza ili kuangalia kama TFF wataruhusu kuongeza wachezaji nane au kumi wa kigeni. Tumeelezwa ni mchakato unaoendelea.“TFF wakisema wanaongeza, mara moja Ngoma anakuja Dar es Salaam kusaini. Unajua baada ya Coutinho na Sherman kutemwa zimebaki nafasi mbili ziko wazi.

“Lakini inaonekana inabidi kusubiri kocha pia aseme maana ameachiwa nafasi hizo mbili kwa kuwa anatakiwa kuja na fowadi mmoja na beki mmoja wa kati.“Kidogo hii inachanganya ndiyo maana tumeamua Ngoma abaki Zimbabwe kwa muda tukiendelea kuangalia hii hali,” kilieleza chanzo kutoka ndani ya Yanga.

Ngoma amekuwa mshambuliaji tishio na tegemeo katika kikosi cha FC Platinum pamoja na Zimbabwe. Timu yake iling’olewa na Yanga katika michuano ya Kombe la Shirikisho.Hata hivyo, safu ya ulinzi ya Yanga, ililazimika kufanya kazi ya ziada kuhakikisha inamzuia akiwa kwao ili asiimalize.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.