Monday, April 27, 2015

Anonymous

Wasauzi wamfuata Simon Msuva wa Yanga Dar

Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Simon Happygod Msuva.
Nicodemus Jonas, Dar es Salaam UNAKULA ulichopanda! Ndiyo kauli pekee inayofaa kutumika unapomzungumzia winga tishio msimu huu, Simon Happygod Msuva anayenukia kiatu cha ufungaji bora ambaye tayari ameshawatoa udenda Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini ambao Ijumaa walikuwa uwanjani hapo kumfuatilia kwa ukaribu kabla ya kuweka ‘kikao’ na uongozi wa Yanga muda mfupi baada ya mchezo kati ya Yanga na Ruvu Shooting.

Simon Msuva (kulia) akiwa na Mrisho Khalfani Ngasa.
Msuva amekuwa tishio tangu kuanza kwa msimu huu, ambapo alianza kutikisa kwenye Kombe la Mapunduzi na kutwaa kiatu cha ufungaji bora, kabla ya moto huo kuuhamishia kwenye ligi kuu, ambapo kiatu hicho kinanukia kwake kutokana na mabao yake 16 kuonekana kutofikiwa kirahisi. 

Anafuatiwa na Amissi Tambwe, mwenye mabao 11.
Katika mchezo na Ruvu Ijumaa, winga huyo alifunga mabao mawili kwenye ushindi wa mabao 5-0. Mara baada ya mchezo, jamaa mmoja ambaye alionekana kutofahamu Kiswahili hata kidogo, alikuja na kumuulizia Msuva, baada ya kumpata alianza kumtafuta kiongozi yeyote wa Yanga ndipo alionyeshwa katibu Dk Jonas Tiboroha ambapo walikuwa na mazungumzo ya muda mrefu usiopungua nusu saa.


Msuva akiwasalimia mashabiki (hawapo pichani) katika moja ya mechi ya Ligi kuu Bara.
Championi Jumatatu ilikuwa shuhuda wa tukio hilo na kunasa kila kilichokuwa kikiendelea katika ‘kikao’ hicho, ndipo ikabainika kuwa kiongozi huyo aliyekuwa amevaa jezi ya Kaizer Chiefs ni wakala wa kimataifa wa timu hiyo inayoshiriki ligi kuu nchini humo (ABSA). 

Wakala huyo alisikika akisema kuwa Msuva ndiye anawafaa, hivyo kama vipi wakutane rasmi kiutawala ili kukamilisha mpango huo, akisisitiza kuwa muda huu ndiyo muafaka kwao.

Baada ya mazungumzo ya wawili hao, Championi lilipojaribu kumdodosa katibu, Dk Tiboroha hakutaka kuliweka wazi jambo hilo na kusema kuwa walikuwa wanazungumzia masuala yao binafsi tu.
“Kuna mambo tulikuwa tunaongea tu mimi na jamaa huyu, ni kweli siyo Mtanzania ila siyo kusema ni suala la kumchukua Msuva,” alisema Dk Tiboroha.

Hata hivyo, habari za kina zilizolifikia Championi ni kwamba mazungumzo yale yalimlenga Msuva baada ya kumvutia wakala huyo.
“Ndiyo kwanza wamekuja, lakini pale (uwanjani) hawakuja rasmi, ila ukweli yule ni wakala wa kimataifa wa Afrika Kusini, kazi yake ni kununua na kuuza wachezaji, sasa naona wamevutiwa zaidi na Msuva. Wamepanga kukutana ‘officially’ ila sijajua itakuwa lini,” alisema mtoa habari wetu.

Kaizer Chiefs ndiyo mabingwa wa ligi kuu nchini Afrika Kusini msimu wa 2012/13, mwaka ambao Yanga pia walitwaa ubingwa, huku ikiwa na rekodi ya kuwa na nyota wengi wanaojulikana kimataifa kama Itumeleng Khune (nahodha), Siphiwe Tshabalala (nahodha msaidizi) na Katlego Mphela ambao walitikisa kwenye Kombe la Dunia 2010.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.