Tuesday, April 21, 2015

Anonymous

#VPL YANGA Kuwakosa Mastaa Hawa Mechi ya Leo

Wakilishi pekee wa nchi waliobaki kwenye mashindano ya kimataifa, timu ya soka ya Yanga, leo inatarajia kushuka dimbani kuikaribisha Stand United ya mkoani Shinyanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika majira ya saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. 

Hata hivyo, Yanga ambayo inaongoza katika msimamo wa VPL leo itawakosa wachezaji wake watatu wa kikosi cha kwanza ambao ni pamoja na nahodha, Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondani na Salum Telela wanaokabiliwa na majeraha. 

Nyota hao watatu jana hawakujumuika na wenzao katika mazoezi ya asubuhi ambayo yalifanyika kwenye Uwanja wa Karume uliopo Ilala jijini.


Akizungumza na gazeti hili jana, daktari wa Yanga, Juma Sufiani alisema nyota hao wote wanasumbuliwa na kifundo cha mguu (enka). 

Alisema kuwa wamepumzika ili wapone vizuri kwa sababu timu yao inakabiliwa na mechi ngumu zaidi huko mbele ikiwamo mchezo wa marudiano wa mashindano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Etoile du Sahel ya Tunisia. 

Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm, alisema kuwa timu yake iko tayari kwa mchezo huo wa leo na imejipanga kuendelea kusaka ushindi ili kuukaribia ubingwa. 

Pluijm alisema wamejiandaa kukutana na ushindani katika mchezo huo kwa sababu wapinzani wao pia wanahitaji pointi ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kubaki katika ligi hiyo ya juu hapa nchini. 

"Mechi zote ni muhimu na ngumu, ndiyo maana tunafanya mazoezi kila siku kwa ajili ya kuandaa wachezaji, kila mchezo una changamoto zake na muhimu ni kujipanga ili kutimiza malengo," alisema kocha huyo anayesaidiwa na Mzalendo, Boniface Mkwasa. 

Aliongeza kwamba mechi za ligi pia zinaisaidia timu yake kujiimarisha na kuwa imara kuwakabili wapinzani wao kwenye mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho wanayoshiriki. 

Alisema hali ya majeruhi ndani ya kikosi hicho haimuumizi kichwa kwa sababu kila mchezaji aliyesajiliwa anaweza kutumikia jukumu atakalokabidhiwa na hatimaye kuhakikisha timu inaibuka na ushindi. 

Yanga itakuwa na faida ya uwanja wake wa nyumbani ambao msimu huu imepoteza mechi moja tu dhidi ya Simba, huku pia ikijivunia rekodi nzuri ya kutofungwa na timu nyingine za VPL katika Uwanja wa Taifa zaidi ya Wekundu wa Msimbazi hao na Azam FC tangu uanze kutumika 2007. 

Hata hivyo, uwapo wa mshambuliaji Mnigeria Abasirim Chidiebere aliyeifungia mabao nane hadi sasa, kitaifanya safu ya Yanga ambayo itawakosa Cannavaro, Yondani na Telela kuwa makini dhidi ya kikosi hicho cha kocha Mganda Mathia Lule.


Lakini pia Stand United nao watahitajika kumchunga zaidi Simon Msuva anayeongoza kwa kufumania nyavu akiwa na mabao 13. 

Katika mechi ya raundi ya kwanza iliyozikutanisha timu hizo Oktoba 26, mwaka jana kwenye Uwanja wa CCM Kambarage, 


Yanga ilishinda 3-0, shukrani zikimwendea Jerry Tegeta aliyetupia mawili pamoja na Mbrazil Geilson Santos Santana 'Jaja' ambaye alifunga moja. 

Yanga inaingia uwanjani ikiwa na machungu ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Etoile du Sahel ya Tunisia, wakati Stand United nayo Ijumaa ikitoka kupata sare kama hiyo nyumbani dhidi ya JKT Ruvu. 


Endapo Yanga itashinda, itakuwa imebakiza pointi sita tu katika mechi zake tatu zilizosalia ili kutawazwa bingwa mpya wa VPL msimu huu bila kujali matokeo ya Azam FC inayoshika nafasi ya pili.  

Kikosi cha Stand United ambacho huu ni msimu wake wa kwanza kushiriki Ligi ya Bara, kiliwasili jijini tangu juzi kwa ajili ya kujiandaa kuwakabili vinara hao wa ligi.


Yanga ndiyo vinara wa ligi kutokana na kuwa na pointi 46 wakifuatiwa na mabingwa watetezi Azam wenye pointi 42 na Simba ni ya tatu wakiwa wamefikisha pointi 35.
CHANZO: NIPASHE

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.