Waziri Kivuli wa Viwanda na Biashara, David Kafulia
ameanika kasoro zilizojitokeza wakati wa manunuzi ya mabehewa 25 ya
mizigo, ambazo zimo ndani ya ripoti ya awali ya uchunguzi uliofanywa na
Mamlaka ya Udhibiti na Manunuzi (PPRA) ambayo pia inazungumzia ununuzi wa mabehewa 274.
Kwa mujibu wa Kafulila, kasoro za msingi
katika manunuzi zilizobainishwa kwenye ripoti hiyo ni namna zabuni
ilivyotangazwa na hata upangaji wa viwango ulikuwa na mapungufu hivyo
kuathiri ubora.
Kafulila aliwaeleza waandishi wa habari
jana jijini Dar es Salaam kuwa, amelazimika kuzungumzia kasoro hizo kwa
sababu leo anasafiri kuelekea Dubai na kuwa serikali iliyopo madarakani,
imebaki hatua za lala salama.
Alisema uchunguzi wa PPRA uliangalia
iwapo taratibu za manunuzi zilizoainishwa katika sheria na kanuni za
manunuzi kama zilizingatiwa na kubainika kuwa mchakato wa ununuzi wa
mabehewa uliofanywa na Shirika la Reli Tanzania (TRL), ulitumia fedha iliyotengwa kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2012/13.
Alisema ripoti hiyo inaonyesha kuwa,
kanuni na taratibu chini ya sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004
ilifutwa na Sheria namba 7 ya mwaka 2011 ambazo ndizo zilitumika katika
manunuzi hayo.
Pia alisema uchunguzi huo umebaini kuwa
nyaraka za zabuni zote mbili zinaelekea kuwa kabla ya kutoa tuzo ya
mkataba kwa mzabuni atayeonekana kukidhi masharti yaliyoainishwa kwenye
nyaraka za zabuni, mzabuni huyo atatakiwa kufanyiwa uchunguzi wa kina
ambao TRL haukuufanya.
“TRL
waliingia mkataba na kampuni ya Hindusthan Engineering and Industries
ya India bila kujiridhisha kuhusu uwezo wake, hivyo ilikiuka kifungu cha
53 cha Sheria ya Ununuzi wa Umma na matakwa ya nyaraka za zabuni ambazo
zilitaka uchunguzi ufanyike,” alisema.
Kafulila alisema PPRA ilibaini kuwa
zabuni hizo zilitangazwa kwenye magazeti ya ndani pekee bila kuyahusisha
na yale ya kimataifa kama inavyoelekezwa kwenye nyongeza ya kwanza ya
sheria ya manunuzi.
Kadhalika, alisema uchunguzi ulibaini
kuwa mikataba yote miwili ilisainiwa Machi 21, mwaka juzi ambapo kwa
mujibu wa mikataba hiyo kifungu namba 3, kinaonyesha mabehewa yalitakiwa
kuwasilishwa katika kipindi cha miezi 12 baada ya kusainiwa mikataba
lakini TRL walichelewa.
Alisema PPRA ilibaini kuwa, menejimenti
ya TRL haikuwa makini kushughulikia maombi ya kuongezewa muda yaliyokuwa
yanawasilishwa na kampuni hiyo.
“Katika
mkataba wa zabuni namba PA/113/2012-13/ME/G/OE/014 kampuni hii
iliwasilisha maombi Juni 13, mwaka jana kuomba kuongezewa muda wa
mkataba hadi Desemba 14, mwaka huo, TRL iliyaidhinisha Juni 16 na muda
wa mkataba uliongezwa hadi Septemba 30,” alisema.
-NIPASHE


Note: Only a member of this blog may post a comment.