Historia hii inasemekana imetoka kwa watu ambao wanamfahamu kwa miaka mingi, kijana huyu aliyefunika vyomb0 vya habari kwa kiwango kikubwa wiki hii.
Kwa mujibu wa maelezo ya watu hao, Scorpion alivyokuwa mdogo alikataa shule mapema, hivyo hakusoma. Taarifa za baba yake mzazi hazifahamiki na mama yake mzazi alifariki siku nyingi, huku akimuacha mwanaye katika malezi ya mdogo wake (mama yake mdogo Scorpion), maeneo ya Yombo Buza jijini Dar Es Salaam.Historia hiyo pia inaeleza kwamba Scorpion alishawahi kufungwa jela, japo haijajulikana alikosa nini na alikaa gerezani gani na kwa miaka mingapi. Jina lake kamili ni Salum Njwope, jina ambalo pia ni la babu yake kwa upande wa baba, na inaelezwa ni mwenyeji wa mkoa wa Shinyanga. Kwa mujibu wa mama yake mdogo, mara siku za nyuma, mara nyingi Scorpion alikuwa akiaga nyumbani saa mbili usiku kuwa alikuwa na kazi ya U-Bouncer katika moja ya Klabu za usiku jijini, kisha kurejea nyumbani Yombo Buza alfajiri, jambo ambalo hatimaye lilikuja kugundulika kwamba si kweli; na kwamba muda huo wa usiku kazi yake hasa ilikuwa kujiunga na makundi ya vibaka ambayo yalikuwa yakiibia watu usiku maeneo ya Buguruni.
Scorpion amewahi kushiriki katika shindano la Dume Challenge mwaka 2013, na kuibuka mshindi. Historia inaeleza pia kuwa amefanya mafunzo ya Karate tangu akiwa mdogo na ni mtu ambaye amejaliwa nguvu za mwili za kuzaliwa nazo, na ujasiri.
Mama yake mdogo ambaye kimsingi ndiye mlezi wake anaeleza kwamba, kijana huyu amewahi kuondoka nyumbani kwao kwa kipindi kirefu bila wao kuwa na taarifa ya alipokuwa akiishi wala shughuli aliyokuwa akifanya lakini baadaye akarejea mwenyewe nyumbani.
Juma hili Scorpion alikamatwa na Polisi jijini Dar Es Salaam kwa tuhuma za kumjeruhi na kumng’oa macho mkazi mmoja wa eneo la Buguruni, katika kitendo kilichoelezwa kuwa ni wizi wa fedha. Chini ni picha za Scorpion katika matukio tofauti tofauti.
Note: Only a member of this blog may post a comment.