Tupo kwenye robo ya tatu ya mwaka 2015, mengi yamekwishatokea na
yanaendelea kutokea. Macho na masikio ya watanzania wengi kwa sasa yapo
kwenye masuala ya kampeni za uchaguzi na pengine hiyo inafanya baadhi ya
mambo kutomulikwa ipasavyo.
Kiburudani pamoja na matatizo sugu yaliyopo kwenye kiwanda chetu,
nchi yetu imefanikiwa kujipenyeza kwenye majukwaa mengi ya kimataifa.
Pamoja na kuwepo vipaji mbalimbali vilivyotumia jitihada zao kujaribu na
vingine kufanikiwa kuipeperusha, vipo vingi vilivyoonesha spidi kubwa
zaidi. Ifuatayo ni orodha ya baadhi ya vipaji hivyo.
Diamond Platnumz
Hakuna ubishi kuwa 2015 huenda ukawa ni mwaka wenye mafanikio makubwa
zaidi kikazi na katika maisha binafsi kwa Diamond. Huu ni mwaka ambao
binti yake aliyegeuka kuwa kichanga maarufu zaidi barani Afrika
alizaliwa.
Wengi tunafahamu ni kwa kiasi gani staa huyu alikuwa na hamu kubwa ya
kuitwa baba na Tiffah amekuwa mtoto wa kwanza kuitimiza ndoto yake
hiyo.
Kinachompa furaha zaidi ni kuzaa na mwanamke aliyemzungumzia kumpenda
zaidi ya anavyoweza kuuelezea umma. Tofauti na mastaa wengine waliopata
watoto, Diamond, mchumba wake Zari na mtoto wao Tiffah wameteka vichwa
vya habari vya magazeti na blogs za Afrika kwa kipindi kirefu.
Tuseme tu kuwa ujio wa mwanae hata kipindi alikuwa bado hajazaliwa, umekuja na neema nyingi.
Huu ni mwaka ambao Diamond amefanya mambo makubwa zaidi
yaliyotambulika katika bara zima. Ameshinda tuzo kibao kuanzia ile kubwa
zaidi ya MTV MAMA na zingine za nchi kama Nigeria, Uganda na kwingineko
huku zikiwepo zingine kibao zinazomngoja.
Mwaka huu amefanikiwa kufanya collabo na wasanii wakubwa duniani
akiwemo Ne-Yo wa Marekani, P-Square, KCEE, Flavour na Iyanya wa Nigeria,
Donald wa Afrika Kusini na wengine. Kuna tetesi zinasambaa pia ambazo
binafsi sijaweza kuzithibitisha kuwa huenda akawa na collabo na Nicki
Minaj.
Ngoma yake Nana imeshika chart kubwa za TV na redio barani kote na
hadi Uingereza (BBA Radio 1 Extra). Ameshiriki kwenye kampeni za
kimataifa zikiwemo One Campaign, The Global Goals na zingine.
Ni msanii wa Afrika Mashariki mwenye show nyingi za kimataifa na
amekuwa akichukua pipa baada ya pipa kuvuka bahari kwenda kutumbuiza.
Mpaka naandika makala hii show yake ya mwisho ilikuwa ni Jumamosi hii
huko Mauritius.
Ndio msanii aliyeingiza fedha nyingi zaidi Tanzania kupitia show,
mauzo ya ringback tones, mirahaba, mikataba ya matangazo na mishe
zingine. Kwa makadirio ya haraka, mpaka mwaka huu unaisha, Diamond
anaweza kuwa ameingiza takriban shilingi bilioni 3???!
Alikiba
Alikiba ataukumbuka sana mwaka 2015 kwa mambo mengi. Kubwa zaidi ni
mvutano kati ya mashabiki wake na wale wa hasimu yake Diamond. Pamoja na
mvutano huo kutengeneza nguvu fulani hasi kwenye kiwanda cha muziki
wetu, tofauti hiyo imemtengenezea Alikiba fursa nyingi za kimaitaifa.
Kwa mara ya kwanza muimbaji huyo wa Chekecha Cheketua ameshiriki
kwenye kipindi cha Coke Studio Afrika na kupata shavu kubwa zaidi la
kuteuliwa miongoni mwa wasanii wachache wa msimu huu kushiriki kwenye
wimbo mmoja na Ne-Yo. Fursa hiyo na kwa msaada wa Jokate Mwegelo, Kiba
atafanya ngoma na rapper wa Nigeria, Ice Prince.
Habari njema zaidi kwa mashabiki wake mwaka huu ni pale Davido alipotangaza ujio wa ngoma aliyoshirikishwa na msanii huyo.
Wimbo wake Chekecha Cheketua umefanikiwa pia kupenya hadi kushika
chart za redio kadhaa za Nigeria. Mwaka huu ametajwa pia kuwania tuzo
kibao za kimataifa. Kwa upande wake naye ameshiriki kwenye kampeni za
kimataifa ikiwemo ile ya kupinga matumizi ya bidhaa zitokanazo na pembe
za ndovu ya Wild Aid.
Vanessa Mdee
Vanessa Mdee kwa sasa anachukua nafasi ya mwanamuziki wa kike kutoka
Afrika Mashariki mwenye mafanikio makubwa zaidi kimuziki. Nobody But Me
aliyomshirikisha rapper K.O. wa Afrika Kusini iliyashawishi masikio ya
wahariri wa jarida maarufu zaidi la masuala ya burudani la Marekani,
Essence na kumjumuisha kwenye toleo lao la kimataifa. Wimbo huo pia
ulishika chart za vituo vikubwa vya runinga vikiwemo MTV Base na Trace
TV.
Pamoja na TV, wimbo huo uliingia kwenye Top 10 za redio za Nigeria, Afrika Kusini na kwingine.
Naye pia ameshirikishwa kwenye collabo kibao za kimataifa ukiwemo
wimbo aliofanya na Pantoraking wa Nigeria, Sayi Shay, Shaydee na
wengine. Ukiachilia mbali kutajwa kuwania tuzo za MTV MAMA mwaka huu,
Vee Money pia ametajwa kuwania tuzo takriban nne zingine za kimataifa.
Mwaka huu alishiriki kwenye wimbo ‘Strong Girls’ wa One Campaign.
Millen Magese
Millen Magese ni mwanamke jasiri na shujaa ambaye tatizo lake la
endometriosis halijamzuia kutoyafurahia maisha yake na kusaidia
wanawake wengine wenye tatizo hilo. Kutokana na kujitangaza hadharani na
kuanzisha taasisi ya kusaidia na kukuza uelewa wa tatizo hilo barani
Afrika, Millen amegeuka kuwa mwanaharakati muhimu barani Afrika.
Harakati hizo mwaka huu zilimfanya atunukiwe tuzo ya kwanza na
heshima ya BET Global Good. Harakati zake pamoja na kutambuliwa hadi
kupewa tuzo, zimemsaidia kwa kiasi kikubwa kuitangaza Tanzania.
Mwaka huu pia Millen alishirikishwa kwenye video ya ngoma ya msanii wa Nigeria, Banky W.
AY
AY ni miongoni mwa wasanii wakongwe ambao kila mwaka huwa na kitu
kikubwa na hata kama wasipohit sana kama wengine. Asipokuwa na hit
single basi lazima atakuwa amepata shavu kubwa la kimataifa analofanya
au kuwa nyuma ya utengenezaji wa kipindi cha TV kilichoshinda mara mbili
kwenye Tuzo za Watu, Mkasi.
Mwaka 2015 umekuwa mzuri sana kwa AY na kwa sababu nyingi tu, AY bado anaendelea kulitetea jina lake la ‘Mzee wa Commercial.’
Video ya wimbo wake ‘Touch Me’ aliomshirikisha Sean Kingston, ilitoka
December 9 mwaka jana lakini Ilipata airtime zaidi mwaka huu. Video
hiyo ilipata mashavu kwenye vituo vikubwa pia vya Afrika ikiwemo MTV
Base na Sound City ambako iliingia kwenye Top 10. Lakini kikubwa zaidi
ngoma hiyo iliingia kwenye charts za redio na TV kadhaa nchini Jamaica.
Video ya wimbo wake ‘It’s Going Down’ aliowashirikisha Lamyia Good wa
Marekani na Ms Triniti nayo ilipata airtime za hapa na pale barani
Afrika.
Mwaka huu AY alikuwa mmoja wa wasanii wa Afrika Mashariki
walioshiriki kama mentors kwenye shindano la Maisha Superstar la Maisha
Magic. Akiwa na rookie, Damian Soul, AY aliongeza kutilia wino wa
umaarufu wake barani Afrika.
Kubwa zaidi ni kuwa AY ni miongoni mwa wasanii waliofanikiwa kuachia
hit single mwaka huu. Zigo iliyotengenezwa na Nahreel haijafanya vizuri
Tanzania tu bali Afrika Mashariki nzima na hadi Nigeria kiasi cha Wizkid
kudaiwa kuwa na mpango wa kufanya remix yake. Jose Chameleone ni
msanii mwingine aliyeonesha nia ya kutaka kuufanyia kitu mdundo wa ngoma
hiyo. Inasubiriwa video yake tu kwa sasa.
Katika kampeni AY ameendelea kushiriki kwenye mambo ya kijamii ikiwa ni pamoja na kuwa balozi wa kujitolea wa UNICEF.
Navy Kenzo
Navy Kenzo ni kundi linaloelekea kuwa miongoni mwa makundi muhimu ya
muziki Afrika. Kundi hilo mwaka huu limefanikiwa kutoa miongoni mwa
video bora za mwaka 2015 ya wimbo wake Game ambao tayari umeshika chart
za redio za Afrika na vituo vikubwa vya runinga.
Lakini hata hivyo ndani ya Navy Kenzo, kuna brand nyingine inayojitegemea – Nahreel.
Nahreel ni producer aliyetengeneza moja ya nyimbo kubwa zilizotoka
mwaka huu, Nana ya Diamond. Tayari producer huyo amekwishafanya kazi za
rappers wa Afrika Kusini, AKA na K.O. pamoja na kundi maarufu la Kenya,
Elani. Mwaka huu alichukuliwa miongoni mwa watayarishaji wa muziki
waliotumika kwenye kipindi cha Coke Studio Africa.
Joh Makini
Joh Makini ni rapper pekee wa Tanzania mwenye video kubwa barani
Afrika, Nusu Nusu. Video ya wimbo huo ilishika hadi nafasi ya kwanza
kwenye chart ya video za Afrika kwenye MTV Base. Haonekani kubweteka na
mafanikio ya video hiyo na ndio maana hivi karibuni alienda tena Afrika
Kusini kushoot video ya collabo aliyofanya na rapper AKA.
Shaa
Miezi ya hivi karibuni Shaa amekuwa kimya kiaina lakini unajua kuwa
ndiye msanii ambaye video yake imeangaliwa zaidi Youtube nchini Tanzania
kama sio Afrika Mashariki?
Sugu Gaga iliyotoka mwaka jana imeangaliwa kwa zaidi ya milioni 19.9
hadi sasa. Mwaka huu Shaa amefanya vizuri na wimbo wake ‘Njoo’
aliomshirikisha Redsan. Video ya wimbo huo ilienda hadi kushika kwenye
Top 10 ya nyimbo za Afrika kwenye kituo cha Nigeria, Sound City. Naye
pia mwaka huu alikuwa mentor kwenye shindano la Maisha Superstar akiwa
nyuma ya rookie, Myra.
Lady Jaydee
Mwaka huu Lady Jaydee aliibuka na tuzo ya mwimbaji wa kike
anayependwa kwenye tuzo za watu. Kimaisha na kibiashara, mambo yake
mwaka huu yameendelea kuwa poa hasa kwakuwa aliwahi kusema kwenye
kipindi chake cha TV ‘Diary of Lady Jaydee’ kuwa ana mpango wa kujenga
nyumba tano mwaka huu.
Kimataifa, mwaka huu Jide alifanikiwa kuingiza video ya wimbo wake
‘Give Me Love’ kwenye chart za MTV Base. Wimbo huo aliwashirikisha
wasanii wa Afrika Kusini, Mazet na Dj Maphorisa wa Uhuru. Mwaka huu pia
Jide alishirikishwa kwenye ngoma mbili na wasanii wa Kenya, Sasa ya Jaya
na Moyo ya Atemi. January mwaka huu alishinda tuzo za Bingwa za Kenya
ambazo ametajwa pia kuwania mwakani.
Wengine?
Sitoacha kuzitambua pia harakati za kimataifa mastaa wengine kama Shettah ambaye ngoma yake Shikorobo aliyomshirikisha Kcee wa Nigeria imemweka pazuri, Hanscana ambaye video alizoongoza ikiwemo Nasema Nawe ya Diamond zimeitangaza Tanzania, Idris Sultan ambaye ushindi wake wa Big Brother Africa ameendelea kuutumia vyema kimataifa na Ommy Dimpoz ambaye video yake ya Wanjera ilishika chart mbalimbali zikiwemo za MTV Base na Sound City.
Wengine ni Yamoto Band ambao video yao mpya ya ‘Cheza Kwa Madoido’ inaelekea kuwapa jina barani Afrika, Sheddy Clever aliyetayarisha wimbo wa Diamond na Ne-Yo, Jux ambaye wimbo wake Looking For You aliomshirikisha Joh Makini umeingia kwenye chart za MTV Base, Ben Pol
ambaye mwaka huu ameshiriki kwa mara ya kwanza kwenye Coke Studio
Afrika na ambaye amesharekodi ngoma na Nameless pamoja na msanii mkubwa
Nigeria, DJ D-Ommy wa Clouds FM aliyechaguliwa kuwa DJ
pekee kutoka Afrika Mashariki kutumbuiza kwenye pre-party ya NBA
AllStars jijini Johannesburg na wengine.
Note: Only a member of this blog may post a comment.