Kijana Geofrey Godian baada ya kunywa sumu.
Na Gladness Mallya, Risasi Jumamosi
DAR ES SALAAM: Kisa 
kinashangaza! Kijana Geofrey Godian (28), mkazi wa Kimara-King’ong’o, 
Dar amenusurika kifo baada ya kunywa sumu kisa kikiwa ni kukataliwa na 
mkewe wa ndoa, Fatma Seleman (23).
Tukio hilo lilijiri wiki iliyopita 
nyumbani kwa wanandoa hao, Kimara-King’ong’o, Dar ambapo Geofrey, baada 
ya kutokea kutoelewana na Fatma kwa kile kilichodaiwa kuwa ana wivu 
uliopitiliza, alifanya jaribio hilo la kutaka kujiua.
mke wa kijana huyo, Fatma Seleman.
Ilisemekana kwamba siku ya tukio, wawili
 hao walikuwa wakigombana ambapo Fatma alimwambia Geofrey hamtaki ndipo 
akaamua kumeza vidonge visivyokuwa na idadi vya malaria viitwavyo Oroda 
ili afe.
Ilielezwa kuwa baada ya kunywa vidonge 
hivyo, hali yake ilikuwa mbaya, akawa anatokwa mapovu mdomoni ambapo 
mdogo wake, Pius Godian alimpa huduma ya kwanza kwa kumnywesha maziwa 
‘freshi’ ndipo akaanza kutapika mfululizo.
Ilisemekana
 kwamba, huku akiwa hajiwezi, alikimbizwa kwenye Hospitali ya Palestina,
 Sinza jijini Dar, baada ya kupewa hati ya matibabu ya polisi (PF-3) 
kutoka Kituo cha Polisi cha Kimara-Mwisho ambapo alipatiwa matibabu na 
kupata ahueni.
Akizungumza na mwanahabari wetu, Fatma 
alisema kuwa yeye na Geofrey wana miaka sita kwenye ndoa na wamejaliwa 
kupata mtoto mmoja wa kike mwenye umri wa mwaka mmoja lakini mumewe huyo
 amekuwa na wivu uliopitiliza huku mara kwa mara wakiwa na migogoro 
ndani ya nyumba kutokana na mwanamke ambaye alizaa na jamaa huyo kabla 
hawajaoana kumfanyia fujo kila wakati.
“Kuna
 mwanamke alizaa na mume wangu kabla hatujaoana, sasa amekuwa 
akinitukana na kunifanyia fujo kwa kushirikiana na marafiki zake kila 
wanaponiona. Pia bado wana mawasiliano mazuri, sasa ni bora aendelee na 
huyo na mimi nimrudie mwanaume wangu wa zamani niliyeachana naye 
niendelee naye maana nimechoka,” alisema Fatma.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa 
Kimara-King’ongo, Demetrius Mapesi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo 
ambapo alisema kuwa alifanya kazi yake ipasavyo ikiwa ni pamoja na kutoa
 taarifa polisi na mke wa Geofrey kufika kituoni kwa ajili ya mahojiano.
“Nilimsikiliza
 mke wa Geofrey na baadaye niliwaacha waende polisi kwa ajili ya PF-3 
(fomu ya matibabu) na kupatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Palestina 
(Sinza) hadi akapona na mke kutoa maelezo Kituo cha Polisi cha 
Kimara-Mwisho,” alisema Mapesi na kuongeza kuwa Geofrey itabidi akajibu 
shitaka la kutaka kujiua.
 

 
 
 
 
Note: Only a member of this blog may post a comment.