Mwana Hip
Hop mkongwe Bongo, Joseph Haule ‘Profesa Jay’ hatimaye wiki hii
alifanikiwa kunyakua kiti cha Ubunge wa Jimbo la Mikumi, Morogoro kwa
tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho alikuwa
akiwania na mgombea kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) bwana Jones Estomih
Nkya.
Ushindi huo wa Professa Jay unalifanya
Bunge la Tanzania kuwa na wanamuziki wawili wakongwe akiwemo Joseph
Mbilinyi ‘Sugu’ ambaye ametetea nafasi yake ya Ubunge katika Jimbo la
Mbeya Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
Gazeti hili liliamua
kumtafuta Professa Jay na
kuzungumza naye juu ya mipango aliyonayo ndani ya jimbo hilo kwa kipindi
cha miaka mitano cha ubunge wake.
Mwandishi: Umepata nafasi uliyoitaka kwa hamu, nini mipango yako kwa wana Mikumi?
Professa Jay: Kitu cha
kwanza kabisa nilichopanga kufanya ni kuwaunganisha wana Mikumi wote.
Najua walionichagua si wana Chadema tu bali hata wa vyama vingine,
wameniamini, hivyo kitu cha kwanza ni kuwaunganisha na kuwakumbusha
kwamba wao ni wamoja.
Mwandishi: Tatizo la maji limekuwa sugu sana Mikumi, unawaahidi nini wananchi katika hili?
Professa J:
Nitahakikisha Jimbo la Mikumi linakuwa na maji safi na salama. Watu
wamekuwa wakitumia maji ya visima, na hata yale safi yanayopatikana si
kwa wingi kama inavyotakiwa, hivyo nitahakikisha kwamba maji safi na
salama yanapatikana kwa wingi.
Mwandishi: Kuna lolote unaweza kuzungumzia kuhusu elimu jimboni kwako?
Professa Jay: Kuna
tatizo kubwa la elimu. Nitahakikisha naleta elimu bora na si bora elimu,
ili elimu bora ipatikane ni lazima muwe na walimu wazuri, vitendea kazi
vingi vya kufundishia lakini vilevile ni lazima tuwe na vitabu vya
kutosha. Shule nyingine hazina vitabu vya kutosha, kama hali itakuwa
hivyo, hatutokuwa na elimu bora, hivyo nitahakikisha vitabu vinapatikana
na walimu wenye ujuzi wanaongezeka.
Mwandishi: Majimbo mengi yamekuwa na tatizo la afya, kwako utalitatuaje hili?
Professa Jay: Nitahakikisha
afya inapewa kipaumbele pia. Tuna hospitali lakini hatuna madaktari wa
kutosha, wanazidiwa nguvu na idadi kubwa ya wagonjwa, nitahakikisha
madaktari wanakuwa wa kutosha lakini pia dawa ni kitu muhimu.
Nisingependa tena kuona hospitali zinakosa dawa, nitahakikisha dawa
zinapatikana vya kutosha.
Mwandishi: Ajira za kutosha hakuna, utafanyaje kulitatua hili jimboni mwako?
Professa Jay: Watu
wasiokuwa na ajira ni wengi sana mitaani. Hili ni janga la taifa lakini
ndani ya jimbo langu nitahakikisha kwamba ajira zinapatikana.
Nitahakikisha nashirikiana na wananchi kuanzisha miradi mbalimbali na
kuwaajiri vijana, pia nitahakikisha kunakuwa taasisi za mikopo kwa ajili
ya kutoa mikopo kwa wajasiriamali na hata wale wanaotaka kufanya
ujasiriamali.
Mwandishi: Utaendelea na muziki au ndiyo mwisho?
Professa Jay: Siwezi
kuacha muziki, nimekulia kwenye muziki ila kwa sasa sitokuwa nikipiga
shoo kama zamani kutokana na majukumu mengi jimboni. Nitawaangalia
vijana wenye kipaji cha muziki jimboni, hao, nitahakikisha wanakua
kimuziki, hata studio yangu ya Mwanalizombe nitaitoa Dar na kuileta
Mikumi ili vijana wa huku wanufaike kimuziki. Kama muziki ndiyo
ulionitoa, basi sitoweza kuuacha mpaka kifo.
Note: Only a member of this blog may post a comment.