Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Cuf, Maalim Seif Sharif Hamad.
Baada ya Ikulu kutoa taarifa ya kukanusha madai ya mgombea urais wa Zanzibar kupitia Cuf, Maalim Seif Sharif Hamad, kuwa ameomba bila mafanikio kukutana na Rais Jakaya Kikwete ili kuzungumzia sakata la kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, mgombea huyo amemuandikia barua rasmi Rais Kikwete akimuomba wakutane ili kuzungumzia hali ya kisiasa ya visiwani humo. Hata hivyo, taarifa fupi ya Cuf iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na kusainiwa na Mkurugenzi wa Cuf, Ismail Jussa Ladhu, hakueleza zaidi juu ya jambo hilo.
Aidha, chama hicho kimesema kufuatia maelekezo ya Rais Kikwete, kimekubali kufanya mawasiliano na wasaidizi wa Rais ili kupanga utaratibu wa kukutana na Mkuu wa Majeshi la Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange, kuzungumzia hali ya usalama ya Zanzibar.
Katika hatua nyingine, jana Maalim Seif alikutana na viongozi wa dini ya Kiislamu na Kikristo wa Zanzibar na kuzungumza nao kuhusu uchaguzi mkuu wa visiwa hivyo uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu na matokeo yake kufutwa kitatanishi na kuwaomba viongozi hao kuingilia kati ili kuhakikisha nchi inabaki na amani na utulivu na maamuzi ya Wazanzibari waliyoyafanya kupitia uchaguzi huo yanaheshimiwa.
Wakati hayo yakiendelea, Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleiman Soraga, aliwataka wananchi wa Zanzibar kuendelea kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki cha mpito cha kusubiri mgogoro huo ukishughulikiwa ili kupata ufumbuzi.
Alitoa wito huo baada ya kikao cha pamoja na Maalim Seif, ambcho kilikuwa chini ya uwenyekiti wa Mufti Mkuu wa Zanzibar Shikh Kabi.
Naye makamu wa kwanza wa rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad alieleza masikitiko yake makubwa kutokana na hali tete iliyopo hivi sasa Zanzibar.
Alisema hali hiyo isipodhibitiwa mapema inaweza kuhatarisha amani ya nchi.
Miongoni mwa viongozi wa dini waliohudhuria kikao hicho ni Askofu Shao wa Kanisa Katoliki la Minara Miwili, Askofu Michael wa Kanisa la Anglikana Zanzibar, Sheikh Thabit Nouman Jongo wa Ofisi ya Mufti wa Zanzibar na mapadri na wachungaji wa makanisa mbalimbali yaliyopo Zanzibar.
SOURCE: NIPASHE
Note: Only a member of this blog may post a comment.