YANGA na Simba zimeshinda mechi zao za katikati ya wiki hii, lakini nyuma ya ushindi huo makocha wa timu hizo hukumbana na mazingira magumu sana.
Mazingira hayo magumu ndiyo yanayozifanya timu zao kuongeza ujuzi na mbinu zaidi kuweza kufanya vizuri.
Yanga sasa ipo kileleni mwa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 15
ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi kama hizo, isipokuwa yenyewe
imezidiwa kwenye mabao ya kufunga na kufungwa.
“Huwa hatuna jinsi kwani hulazimika kubadilisha mbinu zetu za ushindi
kila mara kulingana na hali tunayokutana nayo uwanjani, tazama Simba
walitujazia viungo tukashindwa kupita katikati wakati wa kushambulia.
“Tukacheza pembeni zaidi na tukafanikiwa kushinda (mabao 2-0), mechi
na Mtibwa (Sugar) uwanja haukuwa rafiki kwetu, pia wenzetu walikamia
kupita kiasi, lakini wakati wa mapumziko nilibadili kitu na tukashinda
(mabao 2-0),” alisema Pluijm.
Alisema kutokana na Uwanja wa Jamhuri uliopo Morogoro kutokuwa mzuri
sehemu ya kuchezea, hakutaka wachezaji wake wachezee sana mpira, pia
aliwataka kutokubali kugongana na wapinzani wao na kweli walifanikiwa.
“Naamini tukiendelea kucheza hivi tutaendelea kufanya vizuri katika mechi zetu zinazofuata,” alisema Pluijm.
SIMBA NAO HIVYOHIVYO
Kocha wa Simba, Dylan Kerr, amesema hata yeye anapata ugumu katika
mechi zake lakini huwa hana jinsi zaidi ya kuongeza mbinu za kupata
ushindi kwenye mechi zake.
“Kwa muda mfupi niliokuwa Simba, kuna vitu vingi nimejifunza na kubwa
ni kupaniwa kupita kiasi na timu pinzani katika kila mechi, sasa mimi
kila nikigundua hali hiyo nabadili mbinu na napata ushindi.
“Katika mechi dhidi ya Stand United (Simba ilishinda bao 1-0),
tulianza kucheza 4-4-2, mambo yakawa magumu nikawaelekeza kucheza 4-3-3
tukapata bao lakini nina mfumo wa 4-5-1 pia,” alisema Kerr, raia wa
Uingereza.

Note: Only a member of this blog may post a comment.