“Nimeamua
kugombea tena ubunge kwa sababu najua wananchi wa Gairo wananihitaji,
mafanikio makubwa niliyowaletea katika kipindi chote nilichokuwa mbunge
yamewafurahisha na wanaamini kwamba mimi ndiye mkombozi wao.
“Kwa kipindi chote nilichokuwa
madarakani nimeshafanya mambo mengi ya kuwasaidia wananchi na wao ni
mashahidi wa hilo ndiyo maana wananihitaji nigombee tena.
“Nimefanikisha upatikanaji wa maji
Gairo, tatizo ambalo kwa kipindi kirefu lilikuwa likiwasumbua wananchi
wangu. Nimewezesha wakulima kupata matrekta ambayo wanayatumia kwa
shughuli zao za kilimo na Kituo cha Afya cha Gairo sasa kina chumba cha
upasuaji.
“Barabara zinapitika majira yote na
kiwango cha elimu kimepanda tofauti na kabla sijaingia madarakani, Gairo
ya sasa siyo ile niliyoikuta wakati naingia madarakani na wananchi
wangu ni mashahidi wa hilo,” anasema mbunge wa Gairo anayemaliza muda
wake, Mheshimiwa Ahmed Shabib ambaye ameamua kugombea tena kwa tiketi ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika mahojiano maalum na Uwazi,
Shabib ambaye mbali na siasa pia ni mjasiriamali mkubwa anayemiliki
vitega uchumi vingi, akitoa ajira kwa vijana wengi wa Gairo na sehemu
nyingine Tanzania, anasema ameamua kugombea tena ubunge kutokana na kiu
yake ya kuwaletea wananchi wa Gairo mafanikio.
KWA NINI ANAGOMBEA TENA?
“Nataka kuwaletea maendeleo makubwa
zaidi wananchi wa Gairo, nimeshafanya mambo makubwa ya kimaendeleo
lakini naona bado haitoshi, nahitaji muda zaidi wa kuendelea kuwasaidia
wananchi wangu, ndani ya kipindi kifupi nilichokaa madarakani, tayari
nimetatua kero kubwa zilizokuwa zinawakabili wananchi wangu na bado
nahitaji kuendelea kuwasaidia.
“Ushirikiano walionipa kwa kipindi chote
nilichokuwa madarakani umesababisha hata yale matatizo ya wananchi
ambayo awali yalikuwa yanaonekana kuwa kero kubwa yapatiwe ufumbuzi wa
kudumu,” anasema Mheshimiwa Shabib.
VIPAUMBELE VYAKE NI VIPI?
“Nawaomba wananchi wa Gairo wanipe tena
nafasi ya kuwaongoza kwa sababu kama kawaida yangu, mimi si mtu wa
maneno mengi, nafanya kazi ambayo kila mtu anaiona. Nipo tofauti na
wanasiasa wengi.
“Vipaumbele vyangu ni kuboresha huduma
za afya kwa watu wote hasa kwa akina mama wajawazito, watoto na wazee.
Tayari kituo chetu cha afya Gairo kinafanya upasuaji, madaktari na
manesi wapo wa kutosha na malengo yangu ni kuhakikisha naboresha zaidi
huduma za afya, sitaki kabisa kuona mtu anapoteza maisha kwa sababu
amekosa dawa au huduma. Hilo nitalisimamia kwa vitendo.
“Kipaumbele kingine ni suala la elimu,
nimejitahidi sana kwa kipindi chote nilichokuwa madarakani kuhakikisha
hakuna mwanafunzi anayekaa chini, kuhakikisha kuna walimu wa kutosha na
vifaa vya kufundishia na kujifunzia.
“Nimewezesha Shule ya Sekondari ya Gairo
(G Sec) kuwa na kidato cha tano na sita, kuwa na walimu wa kutosha na
vifaa muhimu. Malengo yangu ni kuhakikisha elimu ya Gairo inazidi
kupanda chati na hilo litawezekana endapo wananchi wangu watanipa tena
ridhaa ya kuwaongoza.
“Suala la maji kwa sasa siyo tatizo
jimboni kwangu lakini naona kama haitoshi, nataka kuhakikisha wananchi
wote mpaka wa vijijini kabisa wanapata maji safi na salama kwa muda
wote. Miradi mikubwa ya kusambaza maji inaendelea kwenye vijiji vyote na
wananchi wangu ni mashahidi wa hilo.
“Kwa upande wa kuwawezesha wananchi
wangu, nataka kuwasaidia wanawake na vijana kupata mikopo na mafunzo ya
ujasiriamali ili waweze kujikwamua kimaisha. Naamini ukimuwezesha
mwanamke basi umeikomboa jamii nzima, hali kadhalika ukimuwezesha kijana
basi umewasaidia wengi ambao wapo nyuma yake.
“Nataka kuwaona wanawake na vijana
wakifanya biashara ndani na nje ya Gairo, fursa zipo nyingi, kuanzia
kwenye kilimo cha kibiashara, ufugaji na sehemu nyingine nyingi,”
alisema Shabib.
ANAWAZUNGUMZIAJE WAPINZANI?
Kutokana na heshima ya uchapakazi na
kuwajali wananchi kwa kuyashughulikia kikamilifu matatizo ya wananchi
wangu, sina wasiwasi kabisa na wapinzani. Kwa kifupi Gairo ni kama
hakuna upinzani kwa sababu hao wapinzani waliopo, hawazungumzii sera zao
badala yake wana kazi ya kuhubiri matusi, chuki na uhasama kwa wananchi
wangu. Watanzania hawataki siasa za namna hiyo, wanataka kusikia sera,
kwa kuwa wao hawana sera wanachoweza ni kutukana majukwaani tu.
“Hata wakipambana vipi hawataweza
kushinda kwa sababu wananchi wangu wanaelewa tofauti kati ya siasa chafu
na siasa za kiungwana. Wanazungumza sana kuhusu mimi hasa kutokana na
biashara zangu zikiwemo za mabasi ya abiria na hoteli. Hawajui kwamba
nilikuwa nafanya biashara hata kabla sijawa mbunge.
“Hata kwa upande wa urais, hakuna chama
cha upinzani kinachoweza kuingia ikulu isipokuwa CCM pekee, wananchi
wawe makini kuchagua watu wenye sifa na vigezo vya kutawala nchi na John
Pombe Magufuli ndiyo chaguo sahihi. CCM Gairo mbele kwa mbele! CCM
Tanzania hakuna mpinzani.
Note: Only a member of this blog may post a comment.